Kalemani-"Mradi Stigler's Gorge haujawahi kusimama na hautasimama"

05Apr 2020
Idda Mushi
 Rufiji
Nipashe
Kalemani-"Mradi Stigler's Gorge haujawahi kusimama na hautasimama"

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani amewaondoa hofu Watanzania kuwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya mto Rufiji wa Julius Nyerere  haujawahi kusimama na hautasimama kabla ya kukamilika, kama iinavyodaiwa na baadhi ya watu.

Na kwamba mvua zinazonyesha katika maeneo mbalimbali nchini pia hazijaathiri shughuli zozote za mradi huo uliokwishakamilisha kazi zake kwa zaidi ya asilimia 78.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Kalemani baada ya kutembelea kwa mara ya 11 mradi huo na kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea na kueleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi ambapo akamuagiza Msimamizi wa Ujenzi huo shirika la Umeme  Tanesco na mkandarasi anayejenga  mradi huo kuhakikisha barabara zote za ndani na nje ya mradi zilizo ndani ya mkataba zinakarabatiwa na kupitika  wakati wote.

Akabainisha msisitizo mkubwa kuhakikisha unafanywa kwa makalavati na madaraja  ili mizigo iweze kupita bila mashaka yeyote na kwamba eneo la Fuga la kushusha mizigo kwa njia yaTreni limekuwa msaada mkubwa  kwa kubeba vifaa na mizigo ya mradi huo wa Umeme na eneo hilo limekuwa ni roho ya mradi huo kwa sasa.

Kalemani ametoa wito kwa Shirika la Reli Tazara kuendelea kushirikiana na Shirika la Umeme nchini(Tanesco) pamoja na TECU kusimamia vizuri njia hiyo.

Aidha amewataka Wakala wa Barabara nchini TANROADS kuanza mara moja ujenzi wa kiwango cha lami  barabara ya kutoka stesheni ya fuga  hadi eneo la mradi ya kilometa 35.8 ili kusaidia uletaji wa vifaa vizito eneo la mradi.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani ameyatembelea maeneo matano katika mradi huo ikiwemo eneo la njia ya kufua Umeme, Eneo la kuhifadhi maji yatakayokwenda kwenye mtambo wa kuzalisha umeme, eneo la kusaga kokoto za mradi na Mtambo wa kufua Umeme utakaokuwa na mashine tisa kwaajili ya shughuli hiyo, akamtaka Mkandarasi kuhakikisha kazi hizo zinakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa wakati.

Katika hatua nyingine Kalemani ameeleza kuwa hivi karibuni amelazimika kurudisha nondo tani zaidi ya elfu mbili zilizoletwa na mkandarasi wa ujenzi huo toka nje ya nchi na kusisitiza malighafi na vifaa vyote vinavyopatikana nchini  kuagizwa ndani ya nchi ikiwemo saruji, nondo,bati na vyakula.

Habari Kubwa