Kamati ya katiba na sheria yaipa kongole OSHA

23Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Kamati ya katiba na sheria yaipa kongole OSHA

KAMATI ya Bunge ya Katiba na Sheria imeeleza kuridhishwa kwake na maboresho yaliyofanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kufanya kazi kubwa katika kuimarisha masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi hapa nchini kupitia uboreshaji wa mifumo yake ya utendaji.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, Naibu wake, Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Andrew Massawe, wakiwa katika kikao ambacho Taasisi chini ya Wizara ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, mara baada ya kuhitimisha kikao cha kamati hiyo kilichopokea na kujadili taarifa kuhusu miundo na majukumu ya taaasisi mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mchengerwa amesema kuwa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu zimefanya vizuri katika kuwahudumia wananchi kwa kipindi cha miaka mita no iliyopita.

Wajumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria wakifuatilia kikao ambacho Taasisi chini ya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu yao.

“Tumekuwa na mfululizo wa vikao vya kamati na tumekutana na Wizara na taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kujadili muundo na majukumu ya ofisi hiyo.Kupitia taarifa zilizowasilishwa tumejionea namna ambavyo utendaji umeboreka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka mitano iliyopita (2015-2020) hivyo tunaipongeza wizara na taasisi zake kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika,” amesema Mchengerwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akifafanua jambo katika kikao cha Kamati ya Katiba na Sheria ambapo Taasisi chini ya Wizara yake ziliwasilisha taarifa kuhusu miundo na majukumu yao.

Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, amesema walitumia kikao hicho kuweka mipango na mikakati ya kuendelea kuzishauri taasisi wanazozisimamia namna bora zaidi ya kuendelea kuboresha utendaji wake.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameipongeza wizara inayoshughulikia masuala ya kazi chini ya Waziri Jenista Mhagama pamoja Taasisi husika ambazo ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kufanya mageuzi makubwa katika mifumo na taratibu zake kiutendaji ambayo yamepelekea kuboresha huduma kwa wananchi.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha taarifa kuhusu muundo  na majukumu ya Taasisi yake mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria.

“Leo tumepata mada nzuri sana kutoka kwa Menejimenti ya OSHA kwa sababu sote tunakwenda kazini ambako athari mbalimbali zitokanazo na mazingira ya kazi ambayo si rafiki zinaweza kutokea hivyo kupitia maelezo hayo tumeona jinsi ambavyo OSHA imejipanga kulinda nguvu kazi ya Taifa letu,” amesema Asha Abdallah Juma ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa upande wake Yahaya Massare, Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na Mbunge wa Manyoni Magharibi, amesema hatua ya OSHA kufuta baadhi ya tozo zake ambazo zilionekana kuwa kero kwa wamiliki wengi wa sehemu za kazi, imepelekea mwitikio mkubwa wa wadau katika kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Habari Kubwa