Kamati Kuu Chadema kukutana kesho Dar

21Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kamati Kuu Chadema kukutana kesho Dar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kikao cha Kamati Kuu ya chama kitakutana kesho jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujadili hatima ya viongozi wao waliokamtwa mkoani Mwanza akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21, 2021 Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, amesema kikao hicho ni mahususi kwa ajili ya kujua hatima ya viongozi hao ambao walishikiliwa kuanzia usiku wa kumakia leo mkoani Mwanza. Amesema viongozi hao walikuwa katika maandalizi ya kuanza kwa kongamnao la kudai katiba mpya, lakini polisi walifika katika hoteli ambayo viongozi hao walifikia na kuwakamata kwa kile polisi walichodai ni kuandaa mikutano isiyo na kibali. Mnyika amesema kwa vyanzo ambavyo chama kimepata ni kwamba Mwenyekiti Mbowe amechukuliwa na kuondolewa ndani ya mkoa wa Mwanza na hivyo ametoa wito kwa wanachama wote nchini kuanza kumtafuta hadi apatikane. “Mpaka muda huu tunazungumza na umma hatufahamu Mwenyekiti Freeman Mbowe alipo na yupo kwenye hali gani na jambo hili tunalitafsiri kama ni utekaji,” amesema Mnyika. “Kamati Kuu ya Chama itakutana kesho na kujadili ni maelekezo gani ambayo kama Chama tunapaswa kutoa kwa wanachama na baada ya kikao hicho tutatoa taarifa kwa umma,” amesema. Mnyika ametoa rai kwa Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi wote ambao wamekamatwa kuachiwa mara moja bila masharti yeyote.

Habari Kubwa