Kamati ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yapigwa msasa

13Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kamati ya Bunge Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yapigwa msasa

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeipiga msasa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa kuipatia mafunzo maalumu yenye malengo mbalimbali hasa katika kutetea maslahi ya Taifa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akijadili jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mussa Zungu Jijini Dar es Salaam

Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo pia yatajikita  katika masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi ili kuwajengea uwezo wabunge wa kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya Kamati na Bunge kikamilifu. 

Akifungua mafunzo hayo ya siku tano Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa kupitia mafunzo hayo kamati itapata ujuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Kamati maslahi ya Taifa, masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi  ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yenu ya Kamati na Bunge kikamilifu.

“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa mtapata fursa ya kuelimishwa juu ya mambo Uchumi wa Buluu, mada itakayotolewa na Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa uchumi wa buluu kutoka Zanzibar ambayo imepiga hatua katika utekelezaji wake,” amesema Balozi Mulamula. 

Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Wizara inaamini kuwa wajumbe wa Kamati na washiriki wote wa mafunzo wataendelea kutumia ujuzi watakaoupata kuishauri Wizara na kuwa Mabalozi wazuri ndani na nje ya Bunge katika kulinda taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Niihakikishie Kamati kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nanyi kikamilifu hasa katika kipindi hiki tunapoandaa Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tunaamini kuwa ushiriki wenu utaiwezesha nchi yetu kuwa wa sera iliyosheheni masuala muhimu yatakayoiwezesha nchi kunufaika,” ameongeza Balozi MulamulaKwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mussa Zungu amesema kamati anayoiongoza inafanya kazi kuwa kwa maslahi mapana ya nchi na kuahidi kuwa vichocheo vya maslahi ya nchi vinalindwa kwa maslahi mapana ya nchi.

“Kamati inatoa ushauri ‘cross-cutting’ kwa maana inagusa kila eneo kwa taifa letu, jambo lolote lile linalohusiana na masuala ya foreign huwa tunashauri, mambo ya ulinzi na usalama…..kwa hiyo inatoa mambo yak echini kwa chini kwa malengo ya kuisaidia serikali,” amesema Zungu

Mafunzo haya muhimu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Chuo cha Diplomasia na yatafanyika kuanzia tarehe 13 – 17 Septemba 2021 jijini Dar es Salaam.