Kamati ya bunge yanena utunzaji kumbukumbu

23Mar 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kamati ya bunge yanena utunzaji kumbukumbu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezitaka taasisi za serikali kutumia Kituo cha Taifa cha Kutunzia kumbukumbu (NDC) chenye hadhi ya juu katika viwango vya ubora na usalama wa taarifa na kumbukumbu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Norman Sigala.

Kamati pia imezitaka taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia kituo hicho kutunza kumbukumbu zao.

Akizungumza katika maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu baada ya ziara ya siku moja kwenye Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na miradi ya mkongo wa taifa na kituo mahiri cha kutunzia kumbukumbu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Norman Sigala, alisema uhai wa TTCL uko mikononi mwa serikali.

Aidha, kamati hiyo imezitaka taasisi zote za umma na binafsi kulipa madeni zinazodaiwa na TTCL kuiwezesha kujiendesha kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na watendaji wa umma.

Mjumbe wa kamati hiyo, Rita Kabati, alisema kukamilika kwa mchakato wa kuondoka kwa Bharti Airtel ndani ya TTCL kunahitaji kwenda sambamba na uwezeshaji wa mtaji kama ilivyofanyika kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Awali Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema ushirikiano mkubwa uliotolewa na kamati hiyo, umewezesha serikali kuchukua hatua na kuwapa nguvu mpya ya kurejea katika nafasi yake.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na serikali kulipa Sh. bilioni 14.7 na kuhitimisha ubia usioridhisha na kampuni ya Bharti Airtel ndani ya TTCL uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Habari Kubwa