Kamati ya Lugumi yaibua madudu sita

28Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kamati ya Lugumi yaibua madudu sita
  • *Hoja tatu zakosa majibu, ripoti kuanza kuchambuliwa kesho

BAADA ya kufanya kazi kwa takribani miezi miwili,

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Charles Kitwanga.

Kamati Ndogo ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mradi wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd na Jeshi Polisi wa kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole (AFIS) kwenye vituo vya polisi nchini, imekamilisha ripoti yake na kuibuka na madudu makuu sita, huku ikishindwa kupata majibu ya maswali muhimu matatu kwa kile kilichodaiwa ni kwasababu ya kukosa mkataba wa wabia hao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Aesh Hilary, jana alishindwa kuthibisha wala kukanusha taarifa hizo na badala yake alisema kuanzia kesho atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia jambo hilo.

Alisema kwamba, jana Kamati Ndogo ya PAC iliyopewa kazi ya kuchunguza jambo hilo ilikuwa inakamilisha ripoti yake na kwamba alitarajia kukabidhiwa jana ama leo. “Ripoti sijapokea bado, ila leo (jana) jioni au kesho asubuhi tutakabidhiwa rasmi na sisi tunatarajia kwamba kesho kutwa (kesho) tutakaa kamati nzima ya PAC kuisoma na kuichambua halafu baada ya hapo tutajua ni nini sasa kinaendelea na kilichobainika,” alisema.

Kamati Ndogo ya PAC iliundwa ili kutafuta ukweli juu ya taarifa ya ripoti ya CAG ambayo ilisema mkataba huo ulikuwa wa Sh. bilioni 37 na kwamba kampuni hiyo ilitakiwa kufunga vifaa hivyo kwenye vituo 108 vya polisi nchini lakini licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 (Sh. bilioni 34) ya fedha zote, vifaa ambavyo vilikuwa vimefungwa na vinafanya kazi vilikuwa 14 tu.

YALIYOIBULIWA

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ndogo ambayo jana ilikutana kwa mara ya mwisho ili kukamilisha ripoti yake, walisema katika uchunguzi wao wamebaini mambo makuu sita, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba baadhi ya mashine hizo licha ya kuwapo kwenye vituo vya polisi, baadhi hazifanyi kazi.

Mmoja wa wajumbe hao alilieleza gazeti hili kuwa, kwenye maeneo mengine mashine hizo hazikuwapo kabisa. Aliongeza kuwa, katika baadhi ya maeneo walibaini kuwa, licha ya kuwa vifaa hivyo vilifikishwa, hakukuwa na makabidhiano rasmi kati ya waliokuwa na kazi ya kuvifunga na vituo husika vya polisi.

“Kwa hiyo ni sawa na kwamba walikuwa wanaenda na kuvitelekeza tu huko,” alisema mjumbe huyo. Mjumbe mwingine alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria za mali za umma, uhai wa kompyuta ni miaka minne, hivyo kwa kitendo cha mashine hizo kutelekezwa kwenye baadhi ya maeneo tangu mwaka 2012 bila kufanya kazi, kimsingi hazipaswi kuendelea kuwapo kwa mujibu wa kanuni za serikali.

“Kwa hiyo mashine zimekufa kabla hata mkataba wenyewe haujaisha, kwa hiyo ni kazi inatakiwa ianze upya,” alisema mjumbe mwingine. Katika kuzunguka huko mikoani, walipata taarifa kwamba, Kampuni ya Lugumi ilitakiwa kupewa vyumba maalum kwenye vituo hivyo vya polisi ambavyo wangevikarabati kisha walitakuwa kufunga mashine hizo.

“Ilitakiwa Lugumi apewe chumba kila kituo cha polisi ili akifanyie ukarabati mkubwa wa kufunga AC (viyoyozi), kuweka marumaru, kupiga rangi na kuweka samani mpya ndiyo wafunge hizo mashine, jambo hili halikufanyika kabisa, yaani ni sawa tu na kwamba walikuwa wanaenda na kuzitelekeza hizo mashine huko,” alisema.

Pia katika kile kinachoonyesha kuwa kwenye maeneo mengi mashine hizo zilikuwa hazijafungwa, baadhi ya wajumbe hao walisema kuna watu walikuwa wanafuatilia ni wapi kamati hiyo inaenda na kisha kufika kabla yake ili wafunge mashine hizo.

“Tukifika tunaambiwa labda jana kuna watu wamefika hapa wameleta kompyuta na wamefanya nini na nini,” alisema mjumbe mwingine.

Alisema walibaini pia kwamba, kwenye maeneo mengine ambako vifaa hivyo vipo, havifanani na vingine, jambo hilo lililoleta wasiwasi juu ya uhalali na ubora wake.

Hata hivyo, alisema licha ya kuwa kipengele hicho ni muhimu, kamati hiyo imeshindwa kukifanyia kazi kwa sababu hawakuwa na mkataba ambao ungewawezesha kujua ni vifaa vya aina gani vilitakiwa kununuliwa ili wavilinganishe na vile walivyokuta vimefungwa.

“Kutokana na unyeti wa hili jambo, baadhi ya wajumbe kwenye kamati walikuwa wanavutana sana, hoja yao ilikuwa ni kwamba wameenda kuchunguza vifaa ambavyo hawajui kama ndivyo vilivyotakiwa kufungwa ama laa.

” “Ingawa wajumbe hawa hawakuwa wengi, hoja yao ilikuwa ya msingi kwa sababu lazima ujue kwamba mkataba ulisema kinunuliwe kitu A na ulicho kikuta ni chenyewe au sio chenyewe,” alisema.

MASWALI YALIYOKOSA MAJIBU

Wajumbe hao waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa, katika uchunguzi wao huo wameshindwa kujua namna mchakato mzima wa zabuni ulivyokuwa, kama ulikuwa wa uwazi na uliofuata sheria.

Pia walisema kuwa, wameshindwa kujua kama Sh. bilioni 34 zilizolipwa kwa Lugumi zililipiwa kodi kama ambavyo sheria inataka. Walisema pia kwamba, hawakuweza kubaini endapo thamani ya vifaa hivyo inaendana na fedha zilizotolewa (value for money).

CHIMBUKO LA LUGUMI

Kabla ya kuundwa kwa kamati hiyo ndogo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, iliwasilisha taarifa juu ya utekelezaji wa mkataba huo ambayo ilionyesha kuwa mpango wa kufunga vifaa hivyo kwenye vituo vya polisi ulisukwa baada ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2011/12, ambayo ndani yake ilikuwa na kipengele cha ununuzi wa vifaa maalum (specialized equipment).

“Kutokana na hali ya wakati huo ambapo matukio ya uhalifu wa kutisha na viashiria vya ugaidi vilivyokuwa vimeanza kujitokeza, Jeshi la Polisi liliamua kununua mfumo utakaotumika katika utambuzi wa alama za vidole.

” “Ununuzi wa mfumo huo ulikuwa ni muhimu kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama wa nchi, raia na mali zao.

Kwa kuzingatia unyeti wa kazi iliyotegemewa kufanyika kwa mfumo huu ilibidi kutumia njia ya `single source’ (kutumia mzabuni mmoja bila kushindanisha wengi apatikane mmoja bora), hivyo jeshi hilo lilikaribisha Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kufunga mfumo huo,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ambayo Nipashe imeiona. Inaeleza kuwa, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 204, polisi kupitia kitengo chake cha PMU lilianzisha mchakato wa mfumo huo.

Taarifa hiyo inasema kuwa, Septemba 16, 2011, Bodi Kasimu ya Polisi iliidhinisha uanze mchakato wa manunuzi ya mfumo huo kwa kutumia njia hiyo ya `single source’ na kisha Kampuni ya Lugumi ikapewa nyaraka za zabuni (bid documents).

Pia inaeleza kuwa, Septemba 22, mwaka huo, ufunguzi wa zabuni hiyo ulifanyika na ulihudhuriwa na mwakilishi wa Kampuni ya Lugumi.

Taarifa hiyo inasema, siku iliyofuata (Septemba 23), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, aliteua Kamati ya Tathimini (Evaluation team) iliyokuwa na wajumbe watano.

Siku saba baadaye (Septemba 29), Kamati ya Zabuni iliwasilisha ripoti ya tathimini ambayo ilipendekeza Kampuni ya Lugumi Enterprises.

Ilipofika Novemba 4, taarifa hiyo inasema, bodi Kasimu ya Zabuni ya Jeshi la Polisi, ilifanya kikao na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Tathimini kwa kuiteua kampuni ya Lugumi Enterprises. Baada ya mchakato huo, taarifa hiyo inasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliidhinisha Wizara ya Mambo ya Ndani kuingia mkataba na Kampuni ya Lugumi Enterprises kwa barua yenye kumbukumbu namba JC/A/130/11/1 iliyoandikwa Novemba 25.

Licha ya kuharakishwa kwa mchakato wa kumpata mzabuni bila kumshindanisha, au kujiridhisha na uwezo wake wa kuleta vifaa bora, taarifa hiyo ya polisi inasema mpaka sasa ikiwa ni takribani miaka sita tangu mzabuni alipopitishwa, kwenye baadhi ya maeneo vifaa hivyo havifanyi kazi.

Taarifa hiyo inasema, kwenye maeneo mengi vifaa hivyo havifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa mfumo wa mtandao wa intaneti.

Hali iyo inaendelea kuzusha maswali mengi ikiwa ni pamoja na je, kwa nini walinunua vifaa vinavyotegemea mfumo huo pekee na kupanga kuvifunga nchi nzima wakati walijua kiwango cha upatikanaji wa mtandao nchini?.

Kwa muda mfupi uliotumika kumpata mzabuni bila kumshindanisha, ni kigezo gani kilitumika kuiteua Kampuni ya Lugumi Enterprises na siyo nyingine yoyote? Ikiwa ni miaka takribani sita sasa tangu fedha za kununua vifaa hizo kutolewa na kwenye maeneo mengine bado havijafungwa, viashiria vya ugaidi vilivyotajwa kuwa moja ya sababu ya kuharakisha ununuzi wa vifaa hivyo vimeishia wapi? Wakati ajenda hiyo ilitumika kubariki utolewaji wa fedha haraka.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa