Kamati yaridhishwa na mradi wa maji Litisha Songea

25Apr 2021
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe Jumapili
Kamati yaridhishwa na mradi wa maji Litisha Songea

Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Odo Mwisho imekagua mradi wa maji Litisha wilayani Songea na kuridhishwa.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akimtwisha maji mmoja wa akinababa kwenye kituo cha kutochea maji kwenye mradi ambao unatarajia kunufaisha zaidi ya wakazi 3,000 wa Kata ya Litisha wilayani Songea.

Wanachi wa Kata ya Litisha wameanza kunufaika na huduma ya mradi wa maji, ulioanza kutekelezwa m Mei 29 ,2020 na  unatarajia kukamilika Juni 30,2021

Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji taka na usafi wa mazingira Songea (SOUWASA) Mhandisi Patrick Kibasa amesema mradi huo ulisanifiwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 473,mpaka sasa mradi  huo umekamilika kwa asilimia 70.

Mhandisi Kibasa amesema ujenzi wa mradi huo ni wa kisima chenye urefu wa mita 181 na kina uwezo wa kuzalisha maji lita 9,000 kwa saa ambapo amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi 3,226 wa kata ya Litisha.

Ameitaja miradi mingine ya maji inatarajiwa kujengwa  katika Vijiji vya Litowa,Peramiho (B) na Nakahuga Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia mfuko wa maji wa Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha  Litisha Saidi Hashimu  kwa niaba ya wananchi ameishukuru Serikali kwa kuwajengea mradi huo ambao amesema unakwenda kutatua tatizo kubwa la upatikanaji wa  maji lililokuwa linawakabili kwa muda mrefu.

Mwenyekiti huyo wa kijiji hicho Saidi Hashimu Pia alimpongeza mbunge wa Jimbo la peramiho ambaye pia ni waziri wan chi ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia  ajira, kazi na watu wenye ulemavu na vijana Jenister Mhagama kwa jitiada anazozifanya katika jimbo la peramiho katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya,zahanati, vyumba vya madarasa, miundo mbinu ya barabara pamoja na miradi ya maji,ambapo alimtaji Waziri Jenister Mhagama kuwa ni Transforma ya wananchi wa jimbo la peramiho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma  Oddo Mwisho ametoa wito kwa wananchi kuacha kuhujumu miundo mbinu ya maji kwa makusudi kwani kitendo hicho kinawakosesha  wananchi kupata huduma ya maji.

Mwisho ametoa rai kwa wananchi kulinda vyanzo vya maji na kupanda miti rafiki ya maji ambayo itasaidia vyanzo hivyo kuwa endelevu.

Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema hatamfumbia macho mtu yoyote atakayethubutu kuharibu na kuhujumu miundo mbinu ya maji kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miradi ya maji,hivyo lazima miradi hiyo ilindwe na kutunzwa.

Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Ruvuma imemaliza ziara ya siku tatu kukagua miradi ya maji katika wilaya za Songea na Namtumbo.

Habari Kubwa