Kamati yaridhishwa utendaji NHC

23Jan 2021
Munir Shemweta
Dodoma
Nipashe
Kamati yaridhishwa utendaji NHC

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeridhishwa na kasi ya utekelezaji miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kulitaka shirika kuboresha ubunifu na mikakati ya makusanyo ya malimbikizo ya madeni ya kodi.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk. Maulid Banyani, PICHA MTANDAO

Vilevile, kamati hiyo imeliagiza shirika kufanya ujenzi unaozingatia thamani ya fedha za umma sambamba na kuandaa ripoti ya utekelezaji wa matengenezo ya majengo ya nyumba za shirika, ili kuinua hadhi ya nyumba.

Kamati hiyo imelitaka shirika kuongeza kasi ya ukusanyaji madeni ya kodi za pango la nyumba sambamba na kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali iliyokabidhiwa kuitekeleza.

Shirika hilo pia limepongeza na kamati hiyo kutokana na kasi kubwa katika utekelezaji miradi ya shirika na ile ya kimkakati, hali iliyolifanya kuaminika na serikali na kuongezewa kazi nyingine zaidi za ujenzi.

Akizungumza juzi katika kikao cha kamati hiyo jijini Dodoma, Mwenyekiti wake, Dk. Pius Chaya, alisema NHC inapaswa kuimarisha kipato chake kwa kuhakikisha inakusanya madeni, ili kuwa na utendaji wenye ufanisi na faida kwa shirika.

"Tumeshuhudia shirika likienda kwa kasi nzuri sana hivi sasa kwa kukamilisha miradi iliyokuwa imekwama na pia kujenga miradi mipya ya kimkakati, lakini sisi maagizo yetu kama kamati, tunawataka muimarishe mikakati ya ukusanyaji kodi ili kufanya shirika letu lisonge mbele," aliagiza.

Alilitaka shirika kuimarisha pia uhusiano na halmashauri mbalimbali ili kupata fursa zaidi kama shirika sambamba na kuzisaidia halmashauri katika masuala yanayohusu ujenzi wa nyumba.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dk. Maulid Banyani, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mipango ya shirika kwa kamati katika kikao cha kwanza bungeni.

Habari Kubwa