Kamati za rufaa uchaguzi mdogo kukamilisha kazi leo

09Nov 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Kamati za rufaa uchaguzi mdogo kukamilisha kazi leo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amesema kamati za rufaa za uchaguzi wa serikali za mitaa zitakamilisha kazi yake leo, huku akisisitiza kuwa jina la mgombea likiteuliwa litabaki kwenye katarasi za kupigia kura hata kama amejiengua kushiriki

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo.

Aidha, amesema zaidi ya rufaa 13,500 zimewasilishwa na vyama vyote vya siasa kwenye kamati hizo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Jafo amesema vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo vilipeleka rufaa kwenye kamati za maeneo yao na tayari zingine zimeshatolewa maamuzi.

Aidha amesema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo mtu akiteuliwa jina lake linabaki kwenye karatasi za kupigia kura.

“Jina lako limeteuliwa wewe ukasema labda mimi sishiriki jina lako litakuwa kwenye ‘ballot paper’ kwa mujibu wa kanuni zetu, sasa wewe kupanga ni kuchagua,”amesema.

Amebainisha “Kesho tutapata sura halisi ya mchakato mzima wa uchaguzi haya mapingamizi yamewasilishwa kwenye kamati za rufaa za maeneo husika ambapo mwisho wa kupitia rufaa hizo ni leo na zinafanya kazi kwa mujibu wa ibara ya 23 ya kanuni zetu.”

Akizungumzia ziara aliyoifanya kwa baadhi ya mikoa kupitia kazi zinazofanywa na kamati za rufaa, Jafo amesema alipitia baadhi ya fomu zilizokuwa zimepitiwa na kamati hizo na kubaini kuna makosa kwenye ujazaji fomu.

“Kama vile mtu ameandika umri amezaliwa mwaka 2019, sehemu zingine mtu ameandika hata halmashauri yenyewe haiitwi hiyo msaidizi wa uchaguzi afanye nini?, mwingine sehemu ya saini ameweka tarehe halafu sehemu ya tarehe ameweka saini, fomu zingine mtu amejidhamini mwenyewe, wasimamizi walifanya kazi yao kwa mujibu wa kanuni,”amesema.

Ametaja mapungufu mengine ni kutofautiana majina kwenye fomu na daftari la wapiga kura wa uchaguzi.

“Hivi vyote ni vigezo sehemu zingine ni kama mtu mmoja alichukua fomu akawapa watu wengine ‘wadese’ yaani fomu moja iliyokosewa kundi lote limekosea, hii ni kutokana na viongozi hawakufanya kazi yao vizuri ili fomu zijazwe vizuri,”amesema.

Ameongeza kuwa “Nilishasema malalamiko yote yapelekwe kamati za rufaa kwa kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na hizi kamati hazifungwi na mtu, nashukuru baadhi ya vyama vimewasilisha na kazi inaendelea ya kupitia rufaa hizo ikiwa leo ni mwisho.”

Jafo amesisitiza uchaguzi wa mwaka huu hauna ujazaji holela wa fomu, na kamati za rufaa zitaendelea kupitia na kutoa maamuzi sahihi.

“Kesho tutatoa taarifa ya rufaa zilizopita na watu walioteuliwa kushiriki uchaguzi huo, tunaendelea vizuri tunatarajia leo jioni zitakamilisha kazi kamati za rufaa na zinafanyia kazi rufaa zote kwa kuwa ziliwasilishwa na wagombea, na watatoa matokeo kwa vyama vyote lakini kamati ya rufaa itakuwa imetimiza wajibu wake,”amesema.

Kuhusu mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu, Jafo amesema uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza ukiwa na kanuni bora zaidi ili kila jambo lifanyike kwa utaratibu.

“Wananchi waliochukua walikuwa 555,036 na waliorejesha 539,993 sawa na asilimia 97.29 na asilimia 2.7 hawakurejesha kwasababu mbalimbali,”amesema

Habari Kubwa