Kamati za ujenzi zaonywa, kudhibiti wizi

29Nov 2021
Neema Emmanuel
KWIMBA
Nipashe
Kamati za ujenzi zaonywa, kudhibiti wizi

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amezitaka kamati za ujenzi kuzingatia ujazaji wa fomu kila siku ili kubaini matumizi ya siku hiyo ikiwa ni njia moja wapo ya kudhibiti wizi na upotevu katika ujenzi wa  miradi mbalimbali ya serikali.

Mhandisi Robert amezungumza hayo  wilayani Kwimba katika ziara ya kukagua na kujiridhisha na hali ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya madarasa inalenga kuona jitihada za serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo inayotokana na fedha za kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19.

Amesema ili kudhibiti wizi katika miradi ya serikali fomu hiyo itasaidia kutambua mwenendo wa ujenzi na  kudhibiti upotevu kwa sababu  panapokuwa  na miradi mingi katika eneo kudhibiti ni kitu muhimu hivyo waliainisha  viashiria hatarishi ndio maana wakapata ufumbuzi wa kutoa  fomu inayotakiwa kujazwa kila siku mara baada ya kazi kufanyika.

Pia amesema,fomu hiyo lazima ijazwe na fundi mkuu, mtendaji wa kata au kijiji husika, katibu wa chama, mkuu wa shule na kudhibitisha kwa pamoja matumizi ya vifaa. "Kila kitu lazima waandike na wakianza uchunguzi wataanza na wale waliopo kwenye fomu hivyo wasimamie kwa uadilifu na uaminifu kwa sababu unalipa," amesema na kuongeza kuwa;

"Fomu ijazwe kila siku na itumwe isilazwe kwenye hatua hii ya maboma mkiwa watulivu wiki mbili unaweza kufika mahali pazuri kwenda kwenye hatua za upauwaji pia nina imani mmeanza kutengeneza meza na viti kwa ajili ya shule zote," ameeleza Mhandisi Robert.

Pia amesema mkoa umepokea fedha za kujenga vyumba vya madarasa 985 na kazi inaendelea ingawa  walipata changamoto ya saruji kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Kwimba na Misungwi.

" Nafuatilia taarifa za kila siku na imani Kwimba zaidi ya asilimia 50 mmeanza kuinua maboma,ndani ya siku tatu maboma yote yatakuwa kwenye hatua nzuri, naomba uadilifu na ushikamano uendelee kuwepo ili kukamilisha kwa wakati," ameeleza Mhandisi Robert 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kwimba  Johari Samizi ameeleza kuwa wameinua maboma 51 kati ya 109 kutokana na kuwa nje ya muda wamenunua vifaa kwa aina mbili nje ya viwanda na ndani ya viwanda, changamoto ilikuwa upande wa saruji lakini hadi sasa wanaenda vizuri na wanaimani wataenda na muda uliyowekwa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya  Wilaya ya Kwimba Happiness  Msanga amesema kuwa walipokea fedha kiasi cha  billioni 2.18 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 109, hivyo  wamejipanga kuhakikisha wanasimamia ipasavyo na ujenzi unaendelea kwa kuzingatia ubora pamoja na kufuata taratibu za manunuzi ya bidhaa zitakazohusika kwenye ujenzi huo.

Ameongeza kuwa timu zinashirikiana ipasavyo katika usimamizi na kushauriana ili mambo yaweze kwenda kama yanavyotakiwa,watafanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na matokeo chanya yataonekana kwani madarasa hayo  yatasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuwawezesha kufanya vizuri.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ngudu,ambayo ni miongoni mwa shule zilizopata fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili ,Albanus Tarimo na Mariam Samweli,walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan  huku wakisema  ujenzi huo utawasaidia kusoma kwa uhuru na kuahadi kufanya vizuri katika masomo  .

Mkuu wa Mkoa akiwa wilayani Kwimba ametembelea na kukagua ujenzi katika shule ya sekondari walla,Iseni,Maligisu, Ngudu na Igongwa.

Habari Kubwa