Kamishna akiri changamoto uhifadhi Ngorongoro

12Jun 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Kamishna akiri changamoto uhifadhi Ngorongoro

MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), imesema kuna kitendawili kikubwa ndani hifadhi hiyo kati ya utalii na maendeleo ya binadamu kutokana ongezeko la magonjwa, ujangili na migogoro baina ya wanyama na binadamu.

Kamishana wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi.

Aidha, idadi ya watu na mifugo inayokufa kutokana na ugonjwa wa kimeta, wanyama kuzaliana kizazi hicho hicho inaongezeka, huku mapito ya wanyama yakiendelea kwisha na ifikapo mwaka 2030 hakutakuwa na mapito yanayounganisha hifadhi moja hadi nyingine.

Hayo yalibainishwa jana na Kamishana wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi, alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mkutano wa waandishi wa habari za uhifadhi wa Tanzania na Thailand, walio kwenye programu maalum iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Merekani (Usaid).

Alisema hakuna idadi ya vifo vya binadamu lakini ni wastani wa watu wawili hadi watatu wanafariki dunia  kila mwezi kutokana na kuliwa na wanyama au ugonjwa wa kimeta na kichaa cha mbwa.

Kwa mujibu wa Manongi, hivi karibuni walifanya sensa ya watu ndani ya eneo la Ngorongoro na kubani wameongezeka kutoka 800 hadi 95,000 toka mwaka 1959, huku mifugo ikiongezeka kila siku.

Aidha, alisema hadi Desemba, mwaka jana, zaidi ya ng'ombe 7,500 walikufa kwa kimeta na ukame, mifugo na binadamu ndani ya Ngorongoro wakiongezeka kwa kasi, ikiwamo shughuli za binadamu ambazo haziruhusiwi.

"Haikubaliki mtu kufariki dunia kutokana na magonjwa ya wanyamapori na wala si lengo la uhifadhi na halikubaliki. Lakini hiyo inatokana na ongezeko la watu na mifugo ikiwamo shughuli za binadamu, aina ya nyumba zinazojengwa na sasa ni za kudumu na shughuli za kilimo ambazo hazikubaliki," alisema.

Alisema athari za mwingiliano zinaonekana kwa binadamu kuwa na wanyama na mifugo kuuawa, chakula cha mifugo na wanyama kimepungua na sasa kuna magugu ndani ya hifadhi jambo linalowafanya wananchi wawe maskini zaidi kwa kuwa wanategemea mifugo kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.

"Mamlaka inapata fedha nyingi sana kutokana na utalii lakini hazifanani na maisha ya watu wa eneo husika, tunapata watalii 600,000 kwa mwaka na tulipata zaidi ya Sh. bilioni 120," alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanajiuliza wafanyeje na hali inakuwa ngumu kwamba wanyamapori wanaweza kuishi na binadamu, na kwamba wanapata fedha nyingi kutokana na utalii, lakini maisha ya binadamu yanazodi kuwa magumu, jambo ambalo linawafikirisha kufanya mabadiliko.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa matukio ya uhalifu NCA yana uhusiano moja kwa moja na wananchi wanaoishi ndani ya Ngorongoro, kwa kuwa kati ya waliokamatwa walikuwa ni wanajamii.

Alisema mwaka jana watu nane walikamatwa na nyara za faru ambaye aliuawa kati yake watano ni wanajamii wa Ngorongoro, watatu kutoka nje ya eneo hilo, na kwamba iliuzwa Vietnam.

Habari Kubwa