Kampeni za ACT zatikisa Zanzibar

14Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Kampeni za ACT zatikisa Zanzibar

UZINDUZI wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo jana, uliutikisa mji wa Zanzibar, ambapo umati wa wakazi ulijitokeza katika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, akuhutubia wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika viwanja vya Kibandamaiti Zanzibar jana. PICHA: MTANDAO

Uzinduzi huo uliendana na kampeni za kuwanadi wagombea urais wa Zanzibar, uwakilishi, ubunge na udiwani kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Licha ya jua kali lililokuwa likiwaka, lakini wananchi na wafuasi wa chama hicho walifika mapema majira ya saa nne asubuhi viwanjani hapo, ambapo viongozi wa chama hicho walianza kuzungumza majira ya saa kumi jioni.

Katika viwanja hivyo vilipambwa kwa rangi ya zambarau na nyeupe, huku wasanii mbalimbali wakitumbuiza.

MEMBE AKOSEKANA

Wafuasi wa chama hicho walitarajia kumuona mgombea wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Bernard Membe, kuhudhuria mkutano huo, lakini hakuwapo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, huku ikielezwa kuwa kesho chama hicho kitaendelea na mikutano yake ya kampeni Kisiwani Pemba.

MAALIM SEIF ATAJA VIPAUMBELE

Akiwahutubia wananchi na wapenzi wa chama hicho, mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema akipewa ridhaa atahakikisha Zanzibar inakuwa na katiba mpya yenye maamuzi kamili.

Alieleza kuwa pia atahakikisha anaimarisha uchumi na kutafuta vyanzo vipya vya mapato ikiwamo kujenga bandari mpya na uwanja wa ndege wa kisasa.

Maalim Seif aliwataka vijana ambao hawajaoa kujiandaa kuoa na wale ambao wana mke mmoja kujiandaa kuongeza mke kwa sababu akiingia madarakani uchumi utaimarika.

Alieleza kuwa Zanzibar ina utajiri mkubwa na vyanzo vingi vya mapato, lakini bado hakuna ubunifu wa kuvitumia vyanzo hivyo. “Nikipewa ridhaa na wananchi kuiongoza Zanzibar nitahakikisha tunakuwa na Katiba mpya yenye maamuzi kamili,” alisema Maalim Seif.

Aidha, aliendeleza kauli yake ya kuwa hatokubali kunyang’anywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, na kuwataka wafuasi wa chama hicho kulinda kura zao.

Alieleza kuwa atahakikisha anaboresha sekta ya elimu na kutoa elimu bure hadi chuo kikuu ili nchi iweze kupata wataalamu na kuwa na maendeleo.

Alisema hivi sasa milango ya kwenda ikulu ipo wazi baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kumthibitisha kuwa mgombea kutokana na kuwekewa pingamizi, lakini alishinda pingamizi hiyo.

KAULI ZA ZITTO

Naye Zitto Kabwe alisema kuwa chama hicho kitakaposhinda katika uchaguzi mkuu kitahikikisha kinaunda akaunti ya pamoja kwa ajili ya mapato ya muungano ili Zanzibar iweze kufaidika na mgao wa Muungano.

Aliwataka Wazanzibari kumchagua Maalim Seif ili kuwaletea maendeleo, na kwamba maendeleo hayo hayawezi kupatikana bila ya kuwa na serikali tatu. Alisema ACT itahakikisha inasimamia Katiba mpya ili Zanzibar iweze kunufaika na maendeleo.

Alieleza kuwa watahakikisha kuwa wagombea wao walioenguliwa na tume ya uchaguzi wanarejeshwa na watafanya maandamano kisiwani Pemba kesho.

Habari Kubwa