Kampeni ‘Nyumba ni Choo’ yazindua mashine kunawia

09Jul 2020
Somoe Ng'itu
Ruangwa
Nipashe
Kampeni ‘Nyumba ni Choo’ yazindua mashine kunawia

MASHINE maalumu inayotoa majisafi yanayotiririka imezinduliwa rasmi kwenye Uwanja wa Majaliwa, ulioko katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi wilayani ikiwa ni mwendelezo maalumu wa kupambana na virusi vya ugonjwa wa corona (Covid 19).

Uzinduzi huo umefanyika jana kwa mashabiki walioingia uwanjani hapo kushuhudia mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya wenyeji Namungo FC dhidi ya mabingwa, Simba kutoka jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja Uhusiano wa kampeni ya Nyumba ni Choo, iliyoko chini ya Kampuni ya Project Clear, Kemilembe Mutahaba, alisema wamefanya uzinduzi huo ili kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni.

Alisema kaulimbiu ya mchakato huo ni ‘Usichukulie Poa, Unategemewa’ na hii inalenga kuikumbusha jamii kufikiria kulinda afya zao kwa sababu ya wategemezi wanaowahitaji katika familia zao.

"Kila mtu anategemewa, ana mtu anayemjali, kuna watoto, wazazi, mume au mke, hii inatufanya tuelewe kujilinda sawa sawa na maisha lazima yaendelee hata kama kuna corona," alisema Mutahaba.

Alisema Lindi ni mkoa wa pili kuzindua mradi huo baada ya kufanya hivyo jijini Dar es Salaam na wanatarajia pia kuzindua kwenye mikoa mingine 16.

Aliitaja mikoa itakayofuata ni pamoja na Kagera, Mwanza, Mara, Shinyanga, Mbeya, Iringa, Dodoma, Singida, Tanga, Mtwara, Kilimanjaro, Morogoro na Pwani.

Alisema mradi huo uko chini ya Wizara ya Afya na Nyumba ni Choo wameingia makubaliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika kutekeleza mpango huo kwenye viwanja vyote vinavyochezewa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari Kubwa