Kampeni matumizi ya EFD yarindima 

08Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kampeni matumizi ya EFD yarindima 

MAMLAKA ya Mapato (TRA) imeanza kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) na kuwahimiza wanunuzi kudai na kukagua risiti kila wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kampeni hiyo iliyoanzia Kariakoo, Msimamizi wa Kitengo cha EFD wa Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Hamidu Shaban, alisema jana kuwa kampeni hiyo ni endelevu na inafanyika katika maeneo yote ya Dar es Salaam.

“Tunafanya zoezi hili katika mkoa mzima wa Dar es Salaam kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti kuanzia kwenye mizigo yote inayozalishwa viwandani na kupelekwa madukani, inauzwa kwa risiti na kuhakikisha wale wanaonunua bidhaa wanadai risiti,” alisema Shaban.

Alizitaja adhabu za kutokutoa na kudai risiti kuwa ni faini ya Sh. milioni 1.5 hadi milioni 4.5 kwa wafanyabiashara wasiotoa risiti za EFD na wanunuzi wasiodai risiti adhabu ni Sh. 30,000 hadi milioni 1.5.

Rehema Mbilinyi, mfanyabiashara wa Kariakoo, alibainisha kufurahishwa na kampeni hiyo ya kuhamasisha matumizi ya EFD, akiiomba serikali kugawa makundi ya wafanyabiashara wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuweka viwango tofauti vya kodi ili kuondoa tatizo la baadhi ya wafanyabiashara kutoa risiti pungufu au kutokutoa kabisa kwa kuogopa kuingia kwenye VAT.

“Kampeni hii ni nzuri lakini mimi ninaona kuna haja ya serikali kutoza kodi ya VAT kwa kugawa makundi. Kwa mfano, wale wafanyabiashara wakubwa wawe na asilimia 18 kama kawaida, wafanyabiashara wa kati watozwe asilimia 10 na wasajiliwa wapya wa VAT waanze kwa asilimia tano. 

"Hii itasaidia kupunguza tatizo la kutokutoa risiti au kutoa risiti pungufu,” Rehema aliwasilisha ushauri wake huo kwa TRA.

Sylivanus Nyigu, mfanyabiashara wa Kariakoo, mbali na kuipongeza TRA kwa kampeni hiyo, alisema elimu hiyo itasaidia kuondoa upungufu unaojitokeza kwenye kutoa na kudai risiti na kuutafutia ufumbuzi.

TRA imekuwa na utaratibu wa kufanya kampeni za mara kwa mara kwa lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala yanayohusu kodi, kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za EFD pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa wakati.

 
 

Habari Kubwa