Kampuni 58 zatekeleza agizo la JPM kutoa gawio

12Dec 2019
Augusta Njoji
Nipashe
Kampuni 58 zatekeleza agizo la JPM kutoa gawio

IKIWA zimesalia siku 42 tangu kutolewa agizo na Rais John Magufuli kwa taasisi ambazo hazijatoa michango na gawio kwenye mfuko mkuu wa serikali, Taasisi, Mashirika na Kampuni 58 kati ya 187 zimetekeleza agizo hilo.

Dk.Philipo Mpango

Rais alitoa agizo hilo Novemba 24, mwaka huu Ikulu ya Chamwino baada ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi, kampuni na mashirika 79 kiasi cha Sh.Trilioni 1.05 na kuagiza ndani ya siku 60 taasisi zote ambazi serikali imewekeza zitoe gawio na michango.

Akizungumza baada ya kupokea michango kutoka taasisi mbalimbali, Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philipo Mpango amesema taasisi hizo 58 zimetoa kiasi cha Sh.Bilioni 12.12.

"Nawapongeza kwa kutoa michango yenu huku ndo kuelekea kujitegemea, msimpeleke Waziri wa fedha kwenda kuomba mpelekeni kwenda kukopa, na ili kunipa jeuri hiyo basi ni wajibu wenu mashirika,kampuni na taasisi kutoa michango yenu kwa maendeleo ya Taifa," amesema

Waziri huyo amewapongeza wanaoendelea kutoa michango hiyo kwenye mfuko huo huku akisema anatarajia watoe zaidi.

"Novemba 24 Rais alininong'oneza kuwa Waziri nisiwe mpole, sasa nakumbusha tena kwa makampuni, mashirika na taasisi itakapofika saa sita usiku Januari 23, mwaka 2020, wasipoleta michango bodi zitakuwa zimevunjwa, na hiyo ndo amri ya serikali mchezo umekwisha lazima Tanzania iende mbele,"amesema.

Habari Kubwa