Kampuni ya Simba yaipongeza NIT kuzalisha wataalam

03Dec 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kampuni ya Simba yaipongeza NIT kuzalisha wataalam

KAMPUNI  ya Simba Supply Chain Solutions, imekipongeza Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kwa kuzalisha wataalam katika kada mbalimbali hasa katika kipindi ambacho nchi imejikita katika kuendeleza viwanda na kujenga uchumi imara.

Mkurugenzi wa kampuni ya Simba Supply Chain Solutions, Hussein Dewji kulia akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NIT, Prof. Zacharia Mganilwa, Kushoto na Ajuaye Heri Msese.

Aidha, kampuni hiyo imesema  kwa kipindi kirefu imekuwa ikinufaika na mazao mbalimbali yanayozalishwa NIT katika kupata waajiriwa wenye sifaa na kupata mafunzo mbalimbali kutoka kwa watendaji wao katika ngazi mbalimbali.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hussein Dewji, akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kusaini makubaliano ya kushirikiana na NIT, amesema wanatoa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao, kuajiri wahitimu na kuwapa nafasi ya kujifunza kwa vitendo.

Amesema wameamua kuingia makubaliano hayo na NIT Kwa kuzingatia kuwa kampuni ina zaidi ya wafanyakazi 300 huku asilimia 60 wakiwa ni madereva ambao ni zao la NIT.

"Kutokana na unasaba huo, leo (jana) kampuni yetu  imeingia makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwamo tafiti, mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na mafunzo ya uwezeshaji kwa watendaji. 

Ushirikiano huu unalenga kuziba pengo la ujuzi katika mtiririko mzima wa thamani katika sekta ya usafirishaji na kutengeneza msingi wa maendeleo ya wafanyakazi ili kufikia uboreshaji endelevu, kuongeza tija na ufanisi katika kazi na mifumo na baadae kuongeza vipato vya taasisi zetu na nchi kwa ujumla," amesema Dewji.

Aidha, kuanzia mwaka huu, Kampuni hiyo itakuwa inatoa zawadi kwa wahitimu bora watano wa Stashahada na Shahada katika programu za Uhandisi wa Magari, Usafirishaji na Udereva wa kozi za muda mrefu wa magari ya mizigo.

Dewji ameahidi kuwa, itaendelea kuwekeza katika nyanja mbalimbali na kutoa fursa kwa watanzania wote. 

Habari Kubwa