Kampuni yapewa siku 30 kuhakikisha vijiji 54 vinapata umeme Ushetu

05Dec 2019
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Kampuni yapewa siku 30 kuhakikisha vijiji 54 vinapata umeme Ushetu

WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kalemani(Mb) ametoa siku 30 kwa mkandarasi wa kampuni ya Angelique Internation Co L.t.d kuhakikisha ifikapo Januari 4,mwaka 2020, vijiji vyote 54 viliyopo halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama vinapata nishati ya umeme.

WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani akikata utepe katika moja ya nyumba kata ya Igunda, Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga kama ishara ya uzinduzi wa kuwaunganishia umeme wa rea wananchi jana. PICHA NA SHABAN NJIA

Pia kampuni hiyo ilitakiwa kupeleka nishati ya umeme kwenye vijiji 54 vya Halmashauri ya Ushetu tangu mwaka 2017, lakini mpaka sasa imefanikiwa kupeleka nishati hiyo kwenye vijiji 14 tu.

Kalemani alitoa agizo hilo jana wakati akiwa na ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua mradi wa rea mkoani Shinyanga katika Halmashauri ya Msalala na Ushetu na kusema kuwa, mpaka sasa kati ya makandarasi wanne wa kampuni hiyo watatu ameshawanyanganya hati za kusafiria.

“Mkuu wa wilaya wakandarasi wa kampuni hii wako wanne na kati yao watatu nimeshawanyanganya hati za kusafiria mpaka watakapokamilisha mradi wa rea ambao wanaoutekeleza katika Mkoa wa shinyanga. Hawataweza kurejea nchini mwao India wakamilishe kazi," alisema Kalemani.

Hata hivyo, Kalemani amewataka wakandarasi hao kutoruka vijiji na kubagua nyumba za wananchi wakati wa ufungaji wa umeme na kuongeza kuwa nyumba ya tembe, nyasi, ghorofa, tope pamoja na nyumba za malumalu zote zinahadhi sawa ya kupata umeme.

Aidha alisema kuwa serikali imetoa kiasi cha Bil 16.8 fedha za watanzania kwa ajili ya kupeleka nishati ya umeme vijiji vyote vilivyopo Mkoani Shinyanga, lakini bado mkandarasi yuko nyuma ya muda.

Pia amemtaka mkandarasi kuhakikisha anaongeza kasi ya utendaji kazi na kuhakikisha kabla ya sikukuu ya Krismasi vijiji sita vilivyopo katika kata ya Igunda vinapata umeme na kuhakikisha taasisi zote za umma zinalipia shilingi elfu 27 na kuunganishiwa umeme.

“Kuna tabia ya mameneja na wahandisi wa Tanesco kutokupokea simu wanapopigiwa na wananchi wakati linapotokea tatizo la umeme na akipokea anatoa matusi machafu kwa mwananchi. Ole wenu wenye tabia kama hizo mkiripotiwa tu mnaondolewa kazini,” alisema Kalemani.

Kwa upnade wake, Diwani wa kata ya Kinamapula Sharifu Samweli alisema kuna miradi ya maji ya visima virefu vimerukwa na mkandarasi vinaendeshwa kwa gharama kubwa na ukilinganisha na vingekuwa na nishati ya umeme.

Alisema kuwa, visima hivyo vipo katika kata ya Chambo, makao makuu ya halmashauri ya Ushetu, Nyamilangano, Igunda na Bulungwa, wananchi wanatumia gharama kubwa kuviendesha kwa kutumia umeme wa genereta.

Hivi karibuni Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Ushetu, limemtaka Meneja wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wilayani Kahama kuondoa kampuni ya Angelique Internation Co L.t.d inayopeleka nishati ya umeme kwenye vijiji 54 vya Halmashauri hiyo baada ya kuwa nje ya muda.

Habari Kubwa