Kampuni za simu zaagizwa kujenga minara haraka

25Feb 2020
Futuna Seleman
Kilwa
Nipashe
Kampuni za simu zaagizwa kujenga minara haraka

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amezitaka kampuni za simu za mkononi zilizopewa ruzuku na serikali ya kujenga minara ya mawasiliano ili wananchi wapate huduma hiyo haraka.

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, picha mtandao

Amesema serikali ipo kazini saa 24 katika kutekeleza Ilani ya CCM ili kuhakikisha wananchi wote wa mjini na vijijini wanapata mawasiliano ya uhakika.

Nditiye aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mavuji, Kata ya Mandawa, wilayani Kilwa mkoani Lindi, juzi wakati wa uzinduzi wa mnara wa mawasiliano uliojengwa na kampuni ya simu ya Tigo baada ya kupewa ruzuku na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), kujenga mnara huo ambao amesema hadi sasa asilimia 95.2 ya wananchi wanawasiliana nchini.

"Mawasiliano hayabagui, hayachagui serikali inatoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ajili ya kujenga minara ya mawasiliano ili wananchi waweze kuwasiliana muda wote kwa hiyo mfanye kazi wakati wowote bila kuweka masharti eti hamjajiandaa, serikali ipo kazini, hapa kazi tu," alisema Nditiye.

Alisema serikali inafanya kazi bila kujali itikadi za vyama vya siasa bali inahakikisha wananchi wanawasiliana na serikali inataka wananchi watumie simu kuwasiliana.

“Niwatoe hofu wananchi msiogope maneno yetu ya bungeni ya wabunge wa vyama tofauti wenyewe tukitoka nje ya Bunge tunaongea na kunywa chai pamoja,” alisema Nditiye.

Mwenyekiti wa Bodi wa UCSAF, Dk. Joseph Kilongola, alisema kuwa mfuko huo kwa kushirikiana na wawekezaji, kampuni za simu za mkononi wanahakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na huduma za mawasiliano kwa kuwa ni haki yao.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungala, aliishukuru serikali kwa kujenga mnara wa mawasiliano na kuwa sasa kijiji cha Mavuji wananchi wanawasiliana kwa kupiga simu wanavyotaka tofauti na zamani ilikuwa mpaka wakajitege ili kupata mawasiliano.

Mkurugenzi wa Tigo mikoa ya Pwani, Christopher Mutalemwa, alisema kuwa kampuni za simu zimepata fursa ya kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi baada ya serikali kuunganisha nguvu na kujenga minara kwa kuwa maeneo mengine kampuni za simu haziwezi kupeleka mawasiliano peke yao mpaka washirikiane na serikali.

Habari Kubwa