Kampuni za Ufaransa kuwekeza miradi ya trilioni 9.7/- Tanzania

19May 2022
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kampuni za Ufaransa kuwekeza miradi ya trilioni 9.7/- Tanzania

UJUMBE wa wafanyabiashara 40 wa kampuni kubwa za Ufaransa umeingia nchini kwa lengo la kuweka mipango ya kuwekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 4.2 (sawa na Sh. trilioni  9.76) kwa makubaliano ya sekta za umma na binafsi za Ufaransa.

Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Nabil Hajlaoui (wa pili kushoto), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, wakati alipokutana na wafanyabiashara wa makampuni arobaini kutoka nchini humo wanaotaka kuwekeza hapa nchini. PICHA: JUMANNE JUMA

Hayo yalibainishwa jana na ujumbe wa kampuni hizo uliokuwa nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia Mei 16 hadi jana uliokutana na viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau wengine kwa ajili ya kuangalia fursa na maeneo ya ushirikiano.

Wakizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Balozi wa Ufaransa nchini, Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Afrika ya Shirikisho la Waajiri nchini Ufaransa, Gerard Wolf, alisema kundi hilo ni kubwa kusini na mashariki mwa Afrika kutembelea nchini.

Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui, alisema ugeni huo umekuja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutembelea nchi hiyo Februari mwaka huu na kufanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambao kwa pamoja walikubaliana kushirikiana kwenye sekta mbalimbali.

Wolf alisema kampuni hizo ziko chini ya umoja wao wa Bpifrance, Business France na MEDEF International, ukiwa na wataalamu katika sekta za usafiri, nishati, majisafi, kilimo, chakula na afya zenye lengo la kukidhi mfumo wa ikolojia ya Tanzania ili kukidhi mahitaji ya soko.

“Ziara ya ujumbe huu imechochewa na nia ya dhati ya kampuni za Ufaransa kwa Tanzania, nchi ambayo kutokana na ukuaji wake wa nguvu na utulivu wa kisiasa, inatoa matarajio makubwa ya maendeleo kwa wataalamu wa Ufaransa,” alisema.

“Fursa hizi zinatia matumaini zaidi kwani nchi inajitahidi kurejesha hali ya biashara inayowafaa wawekezaji wa kigeni. Wakati wa mkutano wa viongozi wetu (Samia na Macron), walisisitiza juu ya mageuzi ya biashara bora na kukaribisha kampuni za Kifaransa,” alisema.

Kwa mujibu wa Hajlaoui, Ufaransa inashikilia wadhifa wa urais wa Umoja wa Ulaya, hivyo inakusudia kuisaidia Tanzania kuhamasisha vyombo vya ushirikiano wa Ulaya huku akitolea mfano wa mpango wa Global Gateway wa Euro bilioni 300 katika uwekezaji ili kuipa nchi miundombinu bora na endelevu.

Pia alisema kampuni za Ufaransa nchini zimeongezeka zaidi ya mara tatu kuanzia 12 mwaka 2019 hadi 40 mwaka huu, jambo linalodhihirisha uwapo wa raia wa Ufaransa umepanuka katika biashara ndogo, za kati na kubwa.

Aidha, alisema Ufaransa inatarajia kufadhili awamu ya sita ya ujenzi wa miundombinu ya mwendokasi Dar es Salaam na maeneo mengine nchini ili kuwawezesha Watanzania wa maeneo ya pembezoni kufanya shughuli zao kwa urahisi zaidi.

Kwa mujibu wa Wolf, nchi hiyo iko mbioni kuwa mwekezaji mkuu wa Ulaya nchini kwa kuwa ina nia ya kuongeza ushiriki wake wa moja kwa moja katika miradi ya maendeleo hasa usambazaji na uzalishaji wa nishati kupitia kampuni ya Ufaransa kama vile Total Energie na Maurel & Prom.

Alisema eneo jingine ni usafiri na vifaa kama vile ushirikiano na Airbus na mradi wa kukarabati Terminal II katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Bouygues Batiment International.

“Kampuni za Ufaransa zimejipanga pia katika maeneo mengine kama vile usafi wa baharini (mradi wa Bagamoyo), maji na usafi wa mazingira, mawasiliano ya simu yaliyozinduliwa hivi karibuni na Eurelsat ya huduma yake ya mtandao ya kasi ya satelaiti kupitia kampuni tanzu ya Konnect Broadband Tanzania, afya hospitali ya Dodoma na msaada kwa vituo vya saratani nchini,” alifafanua.

Imeandikwa na Salome Kitomari na Faustine Shija

Habari Kubwa