Kampuni zajitia kitanzi ubanguaji korosho

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
Kampuni zajitia kitanzi ubanguaji korosho

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameshuhudia utiaji saini mikataba ya ubanguaji korosho kati ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania na wenye viwanda vya ndani.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania, Dk. Hussein Mansoor, ndiye aliyetia saini katika hafla hiyo iliyofanyika juzi kwa niaba ya serikali na kampuni nne kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Kampuni hizo ni Hawte Investment Co. Ltd, Micronix Mtwara, Korosho Africa, na Micronix Newala.

Kampuni hizo zimeingia mikataba ya kubangua tani 7,500 wakati Hawte Investment Co. Ltd yenye uwezo wa kubangua tani 2,000 kwa mwaka, imetia saini mkataba wa tani 1,500.

Nayo Micronix Mtwara yenye uwezo wa kubangua tani 2,400 kwa mwaka imeingia mkataba wa tani 1,200 huku Korosho Afrika ya Tunduru mkaoni Ruvuma yenye uwezo wa kubangua tani 5,000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua tani 2,400.

Kwa upande wake, Micronix Newala yenye uwezo wa kubangua tani 5,000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua Tani 2,400.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Hasunga alisema serikali imepitia vifungu vyote vya kisheria kabla ya kuanza kuingia makubaliano na kampuni hizo kwa ajili ya ubanguaji wa korosho.

Alisema kazi ya ubanguaji tayari ilikuwa tayari limeanza kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) ambalo tayari limeajiri wafanyakazi 160.


Hasunga alisema Sido pamoja na majukumu mengine, ilikuwa na kazi mbili ambazo ni kuhakikisha inatengeneza vipuri na mashine mbalimbali ambazo zimeharibika na kuhamasisha wabanguaji wadogo na kuwasajili.

“Baada ya kuwasajili mtatakiwa kuingia nao mikataba kwa kiasi cha korosho wanachokihitaji kwa ajili ya ubanguaji,” alisema Hasunga.


Waziri Hasunga alisema serikali ina matumaini makubwa kuwa mikataba ya ubanguaji iliyotiwa saini itazingatiwa kwa kufuata taratibu na masharti yote kwa mujibu wa sheria.

Alisisitiza kuwa serikali inaingia mikataba na viwanda ambavyo vimekuwa vikibangua korosho kwa muda mrefu, hivyo haina shaka na ubora wa kazi hiyo.


Pia alisema viwanda hivyo vitakuwa na uhakika wa kufanya kazi usiku na mchana kutokana na malighafi nyingi iliyopo tofauti na miaka iliyopita kwa kuwa malighafi ilikuwa haipatikani kutokana na korosho kubanguliwa nje ya nchi.


Hasunga alisisitiza kuwa serikali imeamua kubangua korosho zote nchini ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi sambamba na kuongeza thamani ya zao hilo ili kuuzwa kwa jina la Tanzania na kwamba kwa kufanya hivyo, Wizara ya Kilimo itachangia kwa ufasaha katika uchumi wa nchi.

Habari Kubwa