Kashfa tozo uegeshaji magari Dar

01Jan 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Kashfa tozo uegeshaji magari Dar

UTOZAJI ushuru wa maegesho ya magari jijini Dar es Salaam, umegubikwa na kashfa, baada ya mawakala waliopewa zabuni ya kufanya hivyo, kufanya kazi Zaidi ya muda uliokubalika.

Katika hali ambayo inaonyesha kuna jambo limejificha katika suala zima la ukusanyaji wa ushuru huo, mawakala hao wametoa kauli zinazotofautiana na waajiri wao, ambao ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati jiji kupitia kwa Meya wake, Isaya Mwita, likisema hairuhusiwi kutoza ushuru wa maegesho siku za sikukuu, uongozi wa kampuni ya Ubapa inayokusanya mapato kutokana na maegesho ya magari ikitoa kauli tofauti.

Katika kauli hiyo kinzani, Ubapa wamesema siku za sikukuu wanakusanya mapato hayo mwisho saa nane mchana ingawa na kwamba kuna maeneo mengine ambayo wafanyakazi wao wanakusanya zaidi ya muda huo.

Mwita aliiambia nipashe kwamba katika kipindi cha mapumziko ya sikukuu za umma, utozaji wa ushuru wa maegesho ya magari husitishwa hadi siku za kawaida.

“Sikukuu zote za kitaifa zinazojulikana kisheria utozaji wa ushuru huo husitishwa, kwa kuwa ni siku ya mapumziko kwani hata magari yanayoegeshwa hasa mjini hupungua,” alisema.

Mwita aliongeza kuwa: “Inawezekana Desemba 26 (mwaka jana) ushuru ulitozwa mjini, lakini tarehe hiyo ilikuwa siku ya Jumatatu na watu walikuja kazini na kuegesha magari kama kawaida.”

Katika sikukuu za mwishoni mwa mwaka, hivi karibuni hususan Desemba 26, mwaka huu, Nipashe ilibaini baadhi ya magari kutozwa ushuru huo licha ya kuwa ni mapumziko.

Nipashe ilibaini kwamba mmoja wa wateja waliofika katika hoteli ya Sea Cliff na kupaki gari lake, alitozwa ushuru saa 8:15 mchana na kupewa risiti ya kieletroniki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ubapa, inayosimamia utozaji ushuru wa maegesho ya magari katika Manispaa ya Kinondoni, Richard Chengula, alipoulizwa na Nipashe kuhusu taratibu za utozaji ushuru kwa siku za kazi na za sikukuu, alitofautiana na Meya Mwita.

Chengula alisema siku za sikukuu utozaji wa ushuru kwa magari hufanyika hadi saa nane mchana wakati maeneo ya ufukweni ushuru unatozwa hadi saa nne usiku.

Alisema miongozo ambayo hutolewa na Halmashauri ya Jiji, hutofautiana kulingana na maeneo na kwamba katika siku za Jumamosi na sikukuu, ushuru hutozwa kama kawaida ingawa ni kwa nusu siku.

“Inategemeana na maeneo na maeneo kulingana na mwongozo wa jiji, kwa mfano Kinondoni siku za sikukuu kama Krismasi tunatoza hadi saa nane mchana, isipokuwa katika maeneo ya beach (ufukweni) tunaruhusiwa kuchaji (kutoza) hadi saa nane usiku,” alisema Chengula.

TIKETI ZA KIELEKTRONIKI
Katika hatua nyingine, Mwita alisema kuwa ifikapo kesho (Januari 2, mwaka huu), matumizi ya risiti zisizo za kielektroniki zinazotolewa na wakala wa utozaji ushuru wa maegesho ya magari jijini, zitakoma kwa kuwa zinakwamisha juhudi za ukusanyaji mapato.

Mwita alisema madereva ambao huegesha magari yao na kupewa risiti hizo wazikatae na kudai risiti za kielektroniki.

Alisema wamebainika kuwapo kwa baadhi ya watoza ushuru ambao wamekuwa wakiwapatia risiti madereva zisizo za kielektroniki wanaoegesha magari katika maeneo tofauti jijini.

“Hili ni agizo ambalo nalitoa na tumekwishatoa mara kwa mara kwamba risiti zisizo za kieletroniki ni marufuku, madereva wanaoegesha magari na kupatiwa risiti hizo wasizizikubali, hazitambuliki na fedha yako itakuwa imeenda bure,” alisema Mwita.

Nipashe pia imebaini kwamba kuna mkanganyiko wa utoaji wa risiti hizo, kwa kuwa baadhi ya madereva walioegesha magari hupewa risiti za mashine ya kieletroniki (EFD) na wengine kupewa zisizo za kielektroniki.

Gari lenye namba za usajili T 735 DGL baada ya gari kuegeshwa kwa muda wa saa moja katika mtaa wa Sokoine, Manispaa ya Ilala, lilitozwa ushuru wa Sh. 500 na kupewa risiti isiyo ya kielektroniki yenye namba 426376 ambayo hata hivyo haikukamilika maelezo yake.

Mmiliki wa gari hilo alipomuuliza mtoza ushuru kuhusu tiketi hiyo, hakuwa na majibu ya kutosha zaidi ya kusema hana mashine ya EFD kwa ajili ya kutolea risiti za kielektroniki.

Habari Kubwa