Kasi kisukari yatisha Masasi

17Jul 2019
Hamisi Nasiri
MASASI
Nipashe
Kasi kisukari yatisha Masasi

KASI ya ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo la damu wilayani Masasi mkoani Mtwara, yameonekana kushika kasi kutokana na watu wengi kuwa na mfumo hasi wa ulaji wa vyakula visivyozingatia mahitaji ya mwili.

Kutokana na hali hiyo, wanapokwenda kupima magonjwa hayo hubainika kuwa na kisukari na shinikizo la damu.

Aidha, kutokana na hali hiyo, jamii wilayani humo imeshauriwa kuwa ni vema ikaachana na mfumo hasi wa ulaji wa vyakula vya aina moja kwa muda mrefu ikiwamo kula wanga kupita kiasi, vinywaji vya sukari nyingi kama vile soda, juisi pamoja na vyakula vyenye mafuta mengi.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkomaindo wilayani Masasi, Dk. Rashidi Musa, alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kwa Wilaya ya Masasi.

Alisema katika Wilaya ya Masasi kumekuwa na kasi ya kubwa ya makundi ya watu wenye umri tofauti tofauti likiwamo kundi la wazee wanaokwenda kupima ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo la damu wengi wao kubainika kuwa na magonjwa hayo mawili.

Alisema kutokana na hali hiyo kuwa tishio wilayani hapo, uongozi wa hospitali hiyo inatafuta wadau mbalimbali ambapo wataandaa kampeni ya uhamasishaji jamii kwa kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.

Pia watahamasishwa kuzingatia kula vyakula vya asili badala ya vyakula vya kusindika vya viwandani ili kuepesha kupata magonjwa hayo.

Dk. Rashidi alisema moja ya sababu ambayo inapelekea idadi kubwa ya wananchi wilayani humo kukumbwa na ugonjwa wa kisukari ni mfumo wa maisha wanayoishi hasa ulaji wa vyakula na kutokuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuyeyusha kiwango cha sukari kilichozidi mwilini.

Alisema ugonjwa wa kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari kwenye damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu.

Habari Kubwa