Kata ya Ifulifu yajikongoja ujenzi wa sekondari

26Jul 2021
Sabato Kasika
Musoma
Nipashe
Kata ya Ifulifu yajikongoja ujenzi wa sekondari

KATA ya Ifulifu iliyoko wilaya ya Musoma mkoani Mara, imekuwa ya mwisho kati ya kata 21 za wilaya hiyo, katika ujenzi wa sekondari, huku kata nyingine zikiwa tayari zina shule zake.

Viongozi wa Kata na Kamati ya Ujenzi wakiwa kwenye eneo la ujenzi wa Ifulifu Sekondari, inayojengwa kwenye Kijiji cha Kabegi, Kata ya Ifulifu.

Kwa sasa kata hiyo yenye vijiji vitatu vya Nyasaungu, Kabegi na Kiemba, inaendelea na ujenzi wa sekondari mbili ikiwamo moja ya Kijiji cha Nyasaungu huku vijiji vya Kabegi na Kiemba vikijenga sekondari yake.

Ofisa Eimu Sekondari wa wilaya hiyo, Majidu Karugendo alisema juzi kuwa kata 20 zina sekondari ambazo tayari zilishafunguliwa ikiwamo ya Kata ya Nyamrandirira iliyofunguliwa Julai 5 mwaka huu.

"Kata ya Ifulifu ndiyo pekee haina sekondari yake, lakini wakazi wake wameamua kujenga sekondari mbili kwa wakati mmoja, ambapo Kijiji cha Nyasaungu kinajenga sekondari yake, huku Vijiji vya Kabegi na Kiemba navyo vinakijenga sekondari ya vijiji vyao viwili," alisema Karugendo.

Ofisa elimu huyo alisema, serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa elimu, inaendelea kutatua matatizo ya mrundikano wa wanafunzi madarasani na pia kutosafiri umbali mrefu kufuata elimu.

Alisema, katika jitihada hizo, kwa sasa baadhi ya kata zenye sekondari mbili ikiwamo Kata ya Nyakatende na Nyamrandirira, na kwamba sekondari 10 zinaendelea kujengwa na nyingine zaidi zikiwa mbioni kujengwa.

"Kata ya Ifulifu ni miongoni mwa zile zinazojenga sekondari mbili kwa mpigo, hivyo tuendelee kuwaunga mkono ili wawe na shule zao badala ya wanafunzi kusafiri hadi sekondari ya Kata ya Nyakatende," alisema.

Ofisa elimu hiyo alifafanua kuwa wilaya hiyo ina vijiji 68, na kuongeza kuwa huenda hapo baadaye kila kijiji kikawa na sekondari yake, kwa madai kwamba wananchi wamehamasika na kutambua umuhimu wa elimu.