Katambi afunguka makato miamala ya simu

18Jul 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Katambi afunguka makato miamala ya simu

MBUNGE wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, amewataka wananchi wasilalamike juu ya makato ya miamala ya simu na ongezeko la bei ya mafuta kwa kuwa serikali ina nia nzuri ya kuwaletea maendeleo.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, na Ajira, akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo kwenye mnada wa Oldshinyanga.

Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, na Ajira, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo kwenye mnada wa Oldshinyanga, wakati akila nao nyama choma.

Amesema makampuni ya simu yameingia kwenye mfumo wa kibenki, hivyo serikali imeona ni njia nzuri ya ukusanyaji kodi kupitia makato ya miamala ya simu, ili ipate fedha za  kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Ndugu zangu kupitia makato hayo ya miamala ya simu, kiasi cha fedha kitakacho patikana, ambapo shilingi bilioni 45 zitatengwa kujenga maboma 900, zahanati 500, vituo vya afya 114, maboma 2,500 shule za sekondari, na madarasa 10,000 kwa nchi nzima”

Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,na Ajira, akila nyama choma na baadhi ya wananchi wa Jimbo hilo kwenye mnada wa Oldshinyanga.

"Pia kwa upande wa mafuta zinatengwa shilingi milioni 500 kujenga barabara za ndani nchi nzima , na haya ni machache tu ambayo nimeyasema kuna mambo mengi ambayo yatatekelezwa chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassani," amesema Katambi.

Katika hatua nyingine amewahidi wananchi wa Jimbo hilo, kuwatekelezea ahadi zote ambazo aliwaahidi kipindi cha kampeni, huku zingine akiwa tayari ameshaanza kuzitekeleza.

Nao baadhi ya wananchi wameiomba  Serikali iliangalie vizuri suala hilo la makato ya miamala ya simu, kwa maelezo kuwa lina muumiza mwananchi wa hali ya chini, na ni vyema wagebuni vyanzo vipya vya mapato ili kuwapunguzia ukali wa maisha.

Aidha, hivi karibuni Serikali kupitia Bunge ilipitisha tozo mpya za makato ya simu kupitia miamala ya simu , na kuanza kutumika rasmi Julai 15 mwaka huu, na kuzua mijadala mingi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Habari Kubwa