Katambi aonya wakandarasi wazembe

15Oct 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Katambi aonya wakandarasi wazembe

MBUNGE wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa Madaraja mjini humo, ambapo ameonya Wakandarasi ambao watatekeleza miradi chini ya kiwango.

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi, wapili kutoka kulia, akiangalia ujenzi wa Daraja la Iwelyangula ambalo limekamilika kwa asilimia 100, linalounganisha Kata za Chamaguha na Kitangili.

Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira, amebainisha hayo leo wakati alipomaliza kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa madaraja ya Uzogole, Iwelyangula, na Upongoji.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo kwa Wakandarasi ambao wanapewa kazi mjini Shinyanga, wajipange kisawasawa kutekeleza miradi hiyo kwa kiwango cha juu kulingana na thamani ya fedha (Value for Money).

"Nimekagua ujenzi wa Madaraja Matatu, ambapo nimeona utekelezaji wake, na jingine limeanza kufanya kazi la Iwelyangula, ila naonya Wakandarasi ambao watavurunda kazi zao, hawata pata kazi tena hapa Shinyanga," amesema Katambi.

"Mfano katika Daraja hili la Uzogole- Bugwandege limegharimu Sh.milioni 190, Iwelyangula Sh. milioni 428, na daraja la Upongoji la watembea kwa miguu Sh.milioni 100, ni fedha nyingi na sitakubali zichezewe," ameongeza.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobasi Katambi, ambaye ni ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijna na Ajira, akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Chamaguha, namna walivyokuwa wakipata shida ya kwenda shule mara baada ya daraja la awali kusombwa na Maji.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa fedha, kwa ajili ya utekelezaji wa barabara kwa kiwango cha changalawe, ambapo kwa Shinyanga itapewa jumla ya Sh.bilioni 1.5.

Pia, amesema Serikali imeshatoa Sh.milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Oldshinyanga ,pamoja na Sh.milioni 700, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa kwa shule za Sekondari Manispaa ya Shinyanga.

Aidha, amesema Serikali itapeleka pia vifaa tiba katika kituo cha Afya Kambarage vikiwamo vipimo vya MRA, pamoja na X-RAY, kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobasi Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, akiangalia Daraja la Zamani la Iwelyangula ambalo lilisombwa na maji na kusababisha adha kwa wananchi na wanafunzi hasa katika msimu wa mvua.

Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UWT) Lucy Enock, akizungumza kwa niaba ya Katibu wa Chama hicho Agnes Bashemu, alimpongeza Mbunge Katambi kwa kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo.

Nao baadhi ya wananchi, na wanafunzi ambao wamejengewa Madaraja hayo, akiwamo Mwanafunzi Vailet Adamu, walishukuru ujenzi wake, hasa daraja la Iwelyangula, ambapo la zamani lilisombwa na maji, na hivyo kipindi cha Masika walikuwa wanashindwa kwenda shule.

 

Habari Kubwa