Katavi kujenga hospitali ya waganga wa jadi

11Nov 2019
Kelvin Innocent
Katavi
Nipashe
Katavi kujenga hospitali ya waganga wa jadi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera, amesema kuwa watajenga hospitali kwa ajili ya waganga wa jadi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera, picha mtandao

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na wanahabari na amebainisha kuwa watu walimuelewa vibaya juu ya tamko alilolitoa la kuwataka waganga kuwaroga wananchi ili wakapige kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Homera amesema kuwa kuna baadhi ya watu wanapenda kupotosha ukweli ambao unatokana na kauli ambazo viongozi wanazitoa, ila melekezo walioyotoa kwa viongozi wa dini zote, wazee, machifu pamoja na viongozi wa kimila na waganga wa tiba asilia ni kuwa kwa kutumia maombi yao waombe kwa bidii kubwa ili wapatikane viongozi walio bora nchini hasa katika mkoa huo.

Aidha Homera amesema walikaa na waganga wa tiba asilia wote wa mkoa huo na wameamua kujenga hospitali yao kwa kushirikiana na serikali katika kutoa ushauri juu ya ujenzi wa hospitali hiyo.

“Tunajenga hospitali ya kisasa kabisa ya waganga wa tiba asilia katika mkoa wa Katavi, hospitali itawasaidia waganga hawa kutoka vichochoroni na kuja katika hospitali hii na kila mganga atakaa katika chumba chake cha matibabu anayo shughulika nayo,” amesema Homera.

Hata hivyo amesema hiyo ni fursa kwa waganga wote na hospitali itajengwa katika eneo la Kabungu wilayani Tanganyika ambako ndiko inaelezwa kuna waganga wengi na kata moja inawaganga zaidi ya 1500.

“Maana yake nikwamba tunaelekea kuwatoa kwenye imani za kishirikina na potofu ambazo ni chonganishi zinazo sababisha changamoto mbali mbali. Wiki mbili zilizopita Jaji WiIibrodi Mashauri aliamuru watu kufungwa maisha ambao walikata kiganja cha mtoto albino,” amesma Homera.

Homera amesema serikali itawasajili waganga hao pamoja na kuwapatia elimu ili kuhakikisha wanatoa msaada kwa wananchi na siyo kuendeleza ushirikina na kufanya vitu vya ovyo.

Habari Kubwa