Katavi walia vituo kukosa petroli

14Jul 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Katavi walia vituo kukosa petroli

WAENDESHA vyombo vya moto katika Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi, wameiomba serikali kuingilia kati suala la uuzaji wa mafuta ya petroli kutokana na vituo vingi vya uuzaji wa mafuta hayo kugoma kutoa huduma hiyo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, madereva hao walisema wanapoteza muda mwingi kupanga foleni kusubiri mafuta yanayotolewa na kituo kimoja katika manispaa hiyo.

Doto Julius, dereva wa gari ya kutoka Mpanda kwenda Kasekese, alisema wakienda kununua mafuta kwenye baadhi ya vituo wanaambiwa hawauzi.

"Tunapata shida sana tunaenda kununua mafuta tunaambiwa hawauzi sijui ni kwasababu ya bei hadi ipande hatujui wengine wana mafuta, lakini hawataki kuuza," alilalamika Julius.

Meneja wa Kituo cha Mafuta Sereniva, Thomas Magabe, alisema kituo hicho kwa sasa kimekuwa mkombozi kwa madereva kutokana na vituo vingi kutouza.

Kwa upande wake ofisa huduma kwa wateja na utawala mkoa wa Rukwa, Ramadhan Kakende, alisema taarifa za kukosekana mafuta ndio anazisikia kwa mara ya kwanza na kuahidi kufanya mawasiliano na viongozi wa juu.

Hata hivyo alisema tatizo kama hilo lilitokea baada ya wiki mbili katika Mkoa wa Rukwa na baada ya kufanya utafiti walitambua kuwa wamiliki wa vituo hivyo wanakwamishwa na vituo vikubwa vya mafuta vilivyopo jijini Dar es Salaam, wakituma magari yao wanakataa kuwawekea mafuta.

Habari Kubwa