Katavi wapongezwa kusimamia miradi ujenzi madarasa Mlele

21Jan 2022
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Katavi wapongezwa kusimamia miradi ujenzi madarasa Mlele

KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi kupitia Mwenyekiti wake Beda Katani wameupongeza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Katavi kwa kusimamia kwa umakini na weledi miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe.

-yaliyojengwa kutokana na fedha za Mapambano dhidi ya Uviko 19.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi Beda amesema kitendo Cha Halmashauri ya Mlele kukamilisha Ujenzi wa vyumba vya madarasa na kubakiza ziada ya zaidi ya shilingi Milioni 10,halijawahi kutokea hivyo inaonyesha ni namna gani serikali wamesimamia miradi hiyo kwa uaminifu wa hali ya juu.

Pia ameendelea kusisitiza swala la amani na mshikamano  baina ya Viongozi kuanzia ngazi za juu hadi kwenye shina lengo likiwa ni kushirikiana katika shughuli za Maendeleo kwani pasipo na maelewano Maendeleo hayawezi kupatikana.

Mwenyekiti Beda amewataka Wenyeviti wa serikali za Mitaa kuwasomea wananchi taarifa ya mapato na matumizi ili kuondoa maswali juu ya fedha zilivyotumika na kuona kuwa mchango wao katika kuchangia Ujenzi wa miradi inayoendelea katika Halmashauri hiyo unadhaminiwa.

"wananchi wasomewe mapato na matumizi na kuonyesha ule mchango wao walioutoa wakati miradi hii inaendelea kwa kusogeza tofali,kubeba mchanga,kuchota Maji na mengineyo umedhaminiwa"alisema Mwenyekiti Beda

Mjumbe wa kamati ya siasa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko katika ziara hiyo amesema Shule shikizi ya Msingi Utende imejengwa vyumba vya madarasa 3, Shule ya Sekondari Inyonga vyumba vya madarasa 3 na Shule ya Sekondari Ilela vyumba vya madarasa 2.

Amewataka wanafunzi wa Shule zote tatu kusoma kwa bidii na kuzifikia ndoto zao kwani serikali tayari imekwisha tengeneza miundombinu mizuri ya Elimu kazi ni kwao Sasa kutulia na kusoma.

Nao baadhi ya wajumbe walioambatana na kamati hiyo ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Katavi akiwepo Katibu wa CCM Mkoa Omar Mtuwa amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwa kusimamia kikamilifu Ujenzi wa vyumba vya madarasa 34 vilivyogharimu shilingi Milioni 680.

Habari Kubwa