Katibu tawala ahofia wanafunzi waliofaulu kukutwa na mimba 

06Dec 2019
Marco Maduhu
Shinyanga.
Nipashe
Katibu tawala ahofia wanafunzi waliofaulu kukutwa na mimba 

KATIBU tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, ameingiwa na hofu ya baadhi ya wanafunzi wa kike ambao wamefaulu mkoani humo kujiunga na kidato cha kwanza mwakani (2020), kushindwa kuripoti shuleni kutokana na kuwa na ujauzito.

Katibu tawala mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akitangaza matokeo ya wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha Kwanza Mwakani (2020), kuwa wapo 23,634, wavulana 11,280 na wasichana 12,354.

Imeelezwa mkoa wa Shinyanga umeendelea kukabiliwa na tatizo kubwa la wanafunzi kupewa ujauzito, ambapo mwaka jana (2018) wanafunzi 69 walipewa ujauzito, na mwaka huu (2019) taarifa za mimba mpaka sasa zilizopo ni mimba 120.

Msovela alibainisha hayo leo kwenye kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, kuwa kutokana na mkoa wa Shinyanga kukabiliwa na tatizo la wanafunzi kupewa ujauzito, hivyo ameingiwa na hofu huenda baadhi ya wanafunzi wa kike wasiripoti shule sababu ya kupewa ujauzito.

“Mkoa wa Shinyanga ni kati ya mikoa 13 nchini ambapo wanafunzi wake waliofaulu wote wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, kama mlivyomsikia jana kwenye vyombo vya habari waziri Jafo akitangaza matokeo hayo, ila hofu yangu kubwa sijui kama wanafunzi wote wa kike wataripoti shuleni kama hawata kutwa na ujauzito,”amesema Msovela.

Ofisa elimu Mkoa wa Shinyanga Mohamedi Kahundi, akizungumza kwenye kikao hicho.

“Natoa maagizo kwa maofisa elimu ngazi zote, mfuatilie wanafunzi wote waripoti shule, yule ambaye atakutwa amepewa ujauzito kuchueni hatua na kumfuatilia yule ambaye amempatia ujauzito, na kumpeleka kwenye vyombo vya sheria apate kuchukuliwa hatua kali za kisheria, ili liwefundisho kwa watu wengine,”ameongeza.

Aidha akitangaza wanafunzi waliochanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani mkoani humo kuwa ni 23,634, wavulana 11,280 wasichana 12,354, ambapo waliofanya mtihani walikuwa 30,393 wavulana 14,322, wasichana 16,071, na waliofeli ni wanafunzi 6,759, wavulana 3,042, wasichana 3,717.

Naye mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Nyabaganga Taraba, alisema ili tatizo la mimba za wanafunzi lipate kukoma mkoani humo, ni lazima kila mtu atekeleze majukumu yake, wakiwamo walimu wakuu, watendaji wa vijiji, wazazi, Polisi, madaktari, mahakimu, kwa kuacha kuharibu ushahidi ili watuhumiwa wafungwe jela.

Kwa upande wake Afisa elimu mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi, alidai kusikitishwa na kitendo cha wazazi kuacha kuwapeleka watoto wao wa kike kuishi kwenye shule ambazo zina bweni na kuwapangia Mageto, hali ambayo amedai imekuwa ikichochea tatizo la mimba za wanafunzi.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba, akichangia mada kwenye kikao hicho cha kutangazwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, na kueleza kuchukizwa na kitendo cha wanafunzi kuendelea kupewa ujauzito.

 

Habari Kubwa