Katibu Bunge afunguka Zitto kuanika utajiri wake facebook

31Dec 2017
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Katibu Bunge afunguka Zitto kuanika utajiri wake facebook

SIKU moja baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) kuanika mali zake na madeni kwenye mitandao ya kijamii na kuwataka viongozi wengine wafanye hivyo, Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai, amesema jambo hilo ni uamuzi binafsi wa mtu, hivyo ofisi yake haiwezi kuingilia.

Zitto Kabwe .

Pia katibu huyo aliiambia Nipashe kuwa bado hajauona muswada anaodai Zitto kuwa tayari amewasilisha zaidi ya mara moja kutaka kuwapo kwa sheria itakayowalazimisha wabunge na mawaziri kuweka wazi kwa umma taarifa juu ya mali wanazomiliki pamoja na madeni yao na si taarifa hizo kuishia tu kwa Kamishna wa Maadili.

Juzi, kupitia kurasa za akaunti zake za mitandao ya kijamii ya facebook na tweeter, Zitto aliweka hadharani tamko lake juu ya mali zote anazomiliki pamoja na madeni, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuliwakilisha na kupokewa kwenye Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Jana ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho kisheria kwa kila kiongozi kuwasilisha tamko lake kwenye sekretarieti hiyo.

Katika tamko lake hilo, Zitto alitaja mali zake zinazoweza kuchukuliwa na Watanzania walio wengi kuwa ni utajiri kutokana na hali halisi ya kipato kwa wengi wao.

Mali hizo ni pamoja na fedha taslimu Sh. milioni 55.2 zilizotokana na mshahara; Sh. milioni 21.8 alizoingiza kupitia posho ya kujikimu; Sh. milioni 102 zilizotokana na posho ya ubunge huku posho ya vikao ikiwa sifuri kutokana na ukweli kuwa huwa hachukui.

Kadhalika, Zitto alisema kwa ufupi, tamko lake la mwaka 2017 unaomalizika leo halina tofauti sana na mwaka 2016 isipokuwa katika baadhi ya maeneo ikiwamo kuongezeka kwa deni jipya kutoka Benki ya Azania kiasi cha Sh. milioni 104 na deni la mtu binafsi kiasi cha dola za Marekani 2,300.

Pia kupungua kwa madeni ya benki ya CRDB kutoka Sh. milioni 214 hadi kufikia Sh. milioni 143 na NSSF kutoka Sh. milioni 191 hadi kufikia Sh. milioni 142 baada ya kuyalipa kwa mwaka mzima uliopita; kuongezeka kwa rasilimali ambazo ni hisa 60,000 za kampuni ya Vodacom na kupimwa kwa ardhi eneo la Mangamba Manispaa ya Mtwara Mikindani lenye vitalu 42 vya ukubwa tofauti.

Kuhusiana na uamuzi wa Zitto wa kufichua maslahi yake kwenye kurasa za facebook na tweeter, Kigaigai alisema mbunge huyo hawezi kuzuiwa kufanya hivyo kwa sababu ni uamuzi wake binafsi.

“Hata wewe (mwandishi) ukiamua kufanya hivyo ili mimi nijue, sioni kama kuna tatizo… yeye kaamua (kwa utashi) binafsi na sidhani kama hilo lina kizuizi,” alisema Kigaigai.

Kuhusiana na madai ya Zitto kuwasilisha zaidi ya mara moja muswada wa sheria ya kuwalazimisha wabunge na mawaziri kuweka hadharani tamko la mali zao na madeni kwa nia ya kuimarisha maadili na kufanikisha zaidi dhana ya utawala bora, Kigaigai alisema yeye hajaona muswada huo na wala haufahamu.

“Huo muswada mimi sijauona na wala siujui … katika ofisi hii sina muda mrefu ,” alisema Kigaigai ambaye aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu wa Bunge Oktoba 7, mwaka huu.

 WASOMI WANENAAkizungumzia uamuzi wa Zitto wa kutangaza mali zake na madeni hadharani, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk. Israel Sosthenes, alisema ni sahihi kwa sababu ni jambo zuri kwa viongozi wa umma kutaja mali zao ili zifahamike.

“Ipo faida kubwa ya kutangaza mali tukazijua ili watu waishi kwa uaminifu,” alisema Dk. Sosthenes na kuongeza kuwa uwazi ni mojawapo ya mambo ya msingi katika demokrasia kwa sababu huwezesha ushirikishwaji, kujenga uaminifu na imani kwa makundi mbalimbali.

Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha St. Agustine (SAUT), Mwesiga Baregu, alisema utaratibu uliopo sasa wa urejeshaji fomu unapaswa kuboreshwa kwa sababu licha ya Sekretarieti ya Maadili kupewa taarifa, huwa haiziweki wazi kwa umma.

“Kama ni suala la kisheria na kikatiba wananchi wote wana haki ya kujua… kwa hiyo mimi nakubaliana na Zitto,” alisema Prof. Baregu na kuongeza:

“Mpaka sasa jambo hilo linakuwa kama la kisiasa. Umuhimu wake ni pale tutakapotajiwa mali zao na kama umekubali kuwa kiongozi, lazima ukubali tuyajue mambo yako.’

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Ally Bashiru, alisema anayetaka kuwa kiongozi ni lazima ataje mali zake hadharani ili zijulikane na si kuzificha.

 “Wazitaje … kwani wanaficha nini? Anayetaka kuficha mali zake huyo si kiongozi. Ambaye hana cha kuficha ndiyo awe kiongozi. Ni jambo la mtu kupewa uhuru wa kuchagua ama kuwa kiongozi au usiwe kiongozi, maana ukiwa kiongozi usiwe na cha kuficha na kama unataka kuficha basi usiwe kiongozi,” alisema Dk. Bashiru.