Katibu Chadema wilaya `abwaga manyanga'

21Sep 2016
John Ngunge
Nipashe
Katibu Chadema wilaya `abwaga manyanga'

KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Wilaya ya Arusha Mjini, Lewis Kopwe, ameachia ngazi wadhifa wake.

Hata hivyo, Kopwe amesema uamuzi huo hautokani na ugomvi baina yake na viongozi wenzake.

Akizungumza na wanahabari jijini hapa jana, Kopwe alisema ameachana na wadhifa huo, lakini ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida.

Alisema ameamua kuwaachia wengine nao waendeleze kasi ya kukitumikia chama kama yeye alivyofanya.

"Huu ni uamuzi wa kawaida kabisa na katiba inaruhusu. Niligombea nafasi hiyo na kushinda na lengo lilikuwa kukifikisha chama hapo kilipo. Na kweli kimefika. Sasa hivi tuna madiwani 24 kati ya 25 na
mbunge. Hayo ni mafanikio makubwa," alisema.

Alisema baada ya kujiuzulu kwake, anatarajia kujikita na masuala mengine ya kijamii na kifamilia ingawa ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida.

Habari Kubwa