Katibu Mkuu ACT ajitosa ubunge

14Jul 2020
Stephen Chidiye
Tunduru
Nipashe
Katibu Mkuu ACT ajitosa ubunge

WANACHAMA wawili wa chama cha ACT-Wazalendo, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama katika kinyang'anyiro cha ubunge Tunduru Kaskazini.

Katibu wa ACT-Wazalendo Wilaya ya Tunduru, Fransis Kuvile, alisema jana kuwa mbali na Shaibu, Mwenyejiti wa Jimbo hilo wa ACT-Wazalendo, Usain Mawila, pia amechukua fomu.

Alisema watia nia hao walichukua fomu hizo juzi, akisema nafasi zipo wazi kwa wanachama wanaohitaji kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Kiongozi huyo alisema tayari chama kimesambaza fomu za watia nia wa nafasi za udiwani katika kata zote 39 za majimbo ya uchaguzi ya Tunduru ambayo ni Tunduru Kusini lenye kata 15 na Tunduru Kaskazini lenye kata 24 .

Alisema kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, ACT-Wazalendo imejipanga kusimamisha wagombea katika majimbo yote na kata zake zote.

Katibu Bunge la 11 lililofungwa Juni 16 mwaka huu, ACT-Wazalendo ilikuwa na mbunge mmoja, Zitto Kabwe, aliyekuwa anawakilisha Jimbo la Kigoma Mjini.

Habari Kubwa