Katibu Mkuu aonya malipo ya serikali kufanyika kijima

11Jan 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Katibu Mkuu aonya malipo ya serikali kufanyika kijima

SERIKALI imeziagiza taasisi za umma kuhakikisha zinatumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato ya serikali (GePG), ili kuleta tija katika ukusanyaji wa mapato.

Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, wakati akifunga mkutano baina ya Wizara ya Fedha na idara, wakala wa taasisi na mashirika ya umma yaliyoko Kanda ya Kati, ambayo yameunganishwa na mfumo wa GePG.

Alisema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha mfumo wa GEeG unaleta tija katika ukusanyaji wa fedha za umma, bado baadhi ya taasisi za umma hazijaboresha mifumo yake katika kuandaa ankara.

Alisema taasisi zote za umma zinawajibika kuhakikisha zinaendana na azma hiyo kwa kuboresha mifumo ya kielektroniki inayoandaa ankara ili kuwarahisishia walipaji huduma za serikali kupata ankara zao kwa ufanisi na haraka.

Alisema kwa kufanya hivyo, serikali itakusanya fedha kwa wakati na kutoa huduma bora kwa umma.

"Ili kuhakikisha mfumo wako unafuata viwango stahiki katika kuandaa taarifa ya ankara, hakikisha unawasiliana na idara ya usimamizi wa mifumo ya kifedha," aliagiza.

James alisema taasisi zote za umma nchini zinapaswa kutekeleza matakwa ya waraka namba tano wa Hazina unaozitaka kuhakikisha zinapata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kabla ya kufanya ununuzi, uandaaji, usimikaji na utumiaji wa mfumo wowote wa kielektroniki wa usimamizi wa fedha za umma.

Habari Kubwa