Katibu Mkuu azuia malipo ya mkandarasi

12Jan 2019
Dege Masoli
Handeni
Nipashe
Katibu Mkuu azuia malipo ya mkandarasi

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, amezuia malipo ya Sh. milioni 700 zilizokuwa zilipwe kwa kampuni ya Tango Logistics Limited
inayochimba mabwawa ya Manga, Mkata na Kwandugwa na kuagiza zitumike katika mradi wa maji wa Manga – Mkata.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, picha mtandao

Prof. Mkumbo aliagiza hivyo juzi baada ya mkandarasi huyo kushindwa
kukamilisha mradi wa mabwawa hayo licha ya kulipwa asilimia kubwa ya
gharama, hivyo kusababisha zaidi ya wananchi 22,000 
kukosa huduma hiyo.

Alisema mpango wa serikali wa kutoa maji katika Mto Wami
kupeleka vijiji vilivyoko Wilaya ya Handeni ndio utakuwa ufumbuzi
wa kudumu wa uhaba wa maji wilayani humo na kwamba kuchimba
mabwawa ni sawa na kupoteza fedha.

Akiwa Wilayani hapa, Profesa Mkumbo alisema mradi huo wa
kutoa maji katika Mto Wami, Halmashauri ya Chalinze Wilayani
Bagamoyo kupeleka Handeni utasimamiwa na
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Tanga (Tanga –Uwasa).

“Jukumu la kumpata mkandarasi wa mradi huu imepewa Tanga Uwassa ambayo
hivi karibuni itaendesha mchakato wa kumpata mkandarasi,” alisema Profesa Mkumbo.

Mradi wa uchimbaji mabwawa hayo ulioanza mwaka 2013 na ulipangwa
kukamilika ndani ya miezi sita lakini hadi sasa haujakamilika huku wananchi
wakiwa wanaendelea ya kukosa huduma ya maji safi na
salama.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, alisema mradi
wa kutoa maji Mto Wami kupeleka Mkata kupitia Manga utakuwa ufumbuzi
wa kudumu wa
uhaba wa maji kwa kuwa itakuwa pia rahisi kuyasambaza
kwenye maeneo mengine wilayani humo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe, alisema kwa mujibu wa maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara, Sh. milioni 
700 zitasimamiwa na Tanga-Uwasa kwa ajili ya kutekeleza
mchakato wa uendeshaji wa mradi wa maji wa Manga- Mkata.