Katibu Mkuu CCM akiri kukerwa na mwandishi

16Aug 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Katibu Mkuu CCM akiri kukerwa na mwandishi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amekiri kukerwa na mwandishi wa habari aliyehoji kuhusu elimu yake.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) pembeni ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.

Mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa alionekana mwenye hasira alipokuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki mkutano wa kwanza wa kiongozi huyo wa CCM na wanahabari uliofanyika kwenye ofisi za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam Jumatatu.

Dk. Bashiru alikiri kukerwa na mwandishi huyo alipohojiwa na moja ya vituo vya televisheni jijini Dar es Salaam jana.

Alisema alikuwa na mkutano mzuri na waandishi wa habari na matarajio yake yalikuwa ni fursa muhimu kwake na wanahabari kuwasiliana na umma kuhusu masuala ya CCM yanayofanywa kwa wananchi.

Alieleza kuwa mkutano huo ulikuwa wa kwanza kwake tangu awe Katibu Mkuu CCM na alitoa nafasi ya kuulizwa maswali saba.

"Sikuridhishwa namna mjadala ulivyotokea siku ile, labla pengine wanahabari walikuja wakiwa na matarajio fulani, mimi sikuridhika na nahisi wenyewe hawakuridhishwa pia," alisema.

Dk. Bashiru alisema katika mkutano huo yaliulizwa maswali saba huku akisisitiza kuwa hakupata maswali ya kufikirisha na kudai baadhi ya wauliza maswali ni wanachama wa vyama vya upinzani.

"Bahati mbaya unapojadili masuala ya umma, halafu wanahabari wanachukua mwelekeo wa kiitikadi, kwanza wanawakosesha watazamaji wasaa wa kupata ufafanuzi mzuri," alisema.

"Swali kuhusu katiba lilikuwa linakwaza, namfahamu (mwandishi) ni wa CUF (Chama cha Wananchi) na hii habishi mpaka leo, hata yule wa Tanzania Daima. Swali unalisikia na linakuwa na mwelekeo fulani."

Dk. Bashiru alisema mwandishi wa habari aliyemuuliza swali la Katiba ni mzuri na anamfahamu vizuri na alishajadiliana naye wakati fulani kwenye Ukumbi wa Nkurumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

"Namfahamu vizuri, nafahamu mwelekeo wake wa kisiasa na mimi ni Katibu Mkuu wa CCM, sasa hapa kuna mgongano ambao ukitaka kutumia jukwaa la kuwasiliana na umma kupenyeza hoja ya itikadi ya chama nitajibu hivyo," alisema.

Akimwelezea mwandishi aliyehoji kuhusu elimu yake, Dk. Bashiru alisema alimkera kwa sababu elimu yake kuanzia darasa la kwanza hadi shahada tatu imetokana na fedha za walipakodi.

"Mtu anapohoji uwezo wa kielimu, maana yake anahoji waliokusomesha," Dk. Badru alisema, "mwandishi wa Tanzania Daima alinikera kwa sababu aliwatukana Watanzania kuhoji elimu yangu, sijaitumia vizuri kwa matarajio yake kwamba nimejibu rojorojo.

"Nimesomeshwa na Watanzania tangu darasa la kwanza hadi shahada ya tatu, hii si elimu yangu, ni ya Watanzania. Unapohoji uwezo wa kielimu, unahoji walionishomesha. Nimesoma tangu mwanzo, nilikuwa nawatetea walionisomesha akiwamo yeye na familia yake.

"Muuliza swali hakuwa na sababu ya kuanza swali kwa kuhoji elimu yangu, ndio maana nikawa mkali na sijutii kwa sababu mimi ni kiongozi wa CCM na ni mamlaka yangu.

"Unaponiuliza lazima uwajibike, unaponihoji mimi ni mamlaka ya chama tawala, unaponiuliza lazima uwajibike na swali unalouliza. Kwa mtu ambaye ni mamlaka anawakilisha mamlaka, chama cha wanachama zaidi ya milioni 10, mimi pia ni mwanataaluma, sikuwahi kununua mtihani.

"Sikuwahi kushindwa popote... nina maandishi nimeandika yamekubalika na ubora wake mpaka nimefika hapa nilipo na pengine sehemu ya maarifa yale ndo yamenipa nafasi hii.

"Huwezi kuanza kirejareja kwa sababu umepata nafasi hadharani, kwa sababu ni mwanahabari na umepata nafasi ya kuhoji unaanza kwa swali linalokera halafu utegee... Zitto (Kabwe -- Kiongozi Mkuu ACT-Wazalendo) alinipigia simu akaniambia ningeshuka, hapana nilitakiwa nipande naye lakini sikupata nafasi ningepanda naye zaidi."

Katika mahojiano hayo, Dk. Badru aliulizwa kuhusu uvumilivu wake na akajibu: "Wewe unataka kuuawa, unatakiwa kujitetea usife ili uendelee kujadili, wewe unavumilia? Mtu anatupa ngumi halafu unaiacha ikugonge uvumilie halafu ndo uendelee?"

Alipoulizwa kama swali hilo la elimu lilikuwa gumu kwake, Dk. Bashiru alisema halikuwa swali gumu lakini aliona lilikuwa tusi kwake.

"Apite nilikosoma tangu darasa la kwanza hadi chuo kikuu. Je, unataka nivumilie nini hapo? Uvumilivu una ukomo, alinifikisha mahali ambako kuna ukomo wa uvumilivu," alisema.

"Ninyi ni wanataaluma, mnawajibika zaidi kwa umma kuliko kwa mwajiri wenu, mwajiri akiweka mstari ambao utakushinda kuwajibika kwa umma, unaweza kuacha kazi, kuwajibika kwa umma ni kusema ukweli, kutumia mamlaka kwa maslahi ya wachache dhidi ya wengi, kuchunga ulimi au kalamu yako, hata kama kuna ukweli upime unausema wakati gani."

Dk. Bashiri pia alisema mabadiliko makubwa yaliyofanywa kwa kipindi kifupi CCM na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, ndiyo yaliyomfanya akubali uteuzi wa kushika nafasi hiyo.

"Kama hayo mambo yasingefanyika kabla ya uteuzi wangu, ningesita kukubali au ningekubali shingo upande," alisema.

Dk. Bashiru alisema ameteuliwa Aprili 30, baada ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye ni Rais kufanya mabadiliko makubwa kwa muda mfupi na ya maana kwa taifa.

Habari Kubwa