Katibu Mkuu Kiongozi mpya aona fursa ajira

03Jan 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Katibu Mkuu Kiongozi mpya aona fursa ajira

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemwapisha Zena Ahmed Said, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, huku kiongozi huyo akiahidi kumsaidia Rais kupanua fursa za ajira.

Zena aliteuliwa na Dk. Mwinyi kushika nafasi hiyo mwishoni mwa mwaka jana baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Abdulhamid Yahya Mzee.

Hafla hiyo ya kiapo ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na sekta binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kula kiapo, Zena alisema atakuwa mbunifu katika kumsaidia Rais kiutendaji, ili kufikia malengo ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuteuliwa kwake ni neema kubwa kwake, akiahidi atafanya kazi kwa kufuata kanuni, miongozo iliyopo na kuwa mbunifu katika utendaji kazi wake.

"Jinsi maendeleo yatakapopatikana, ninaamini na ajira zitapatikana, hivyo ninamshukuru Rais kwa kuniteua. Wakati unapotenda kazi, ukiwa na hofu ya kuwa mwanamke utashindwa.

"Nafasi yoyote unapopewa, ifanye kwa weledi wa hali ya juu, acha matendo yako na kazi zako zijisemee," alisema Zena ambaye ameweka rekodi ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza mwanamke Zanzibar.

Alisema wanawake wana majukumu mengi, yakiwamo ya familia, hivyo ni vyema kujali kutekeleza majukumu yao kwa wakati stahiki, ili kazi ziendelee vizuri.

“Mimi kofia hii niliyopewa, nikienda katika familia yangu sitoweza kuivaa, bali nitavaa kofia kama ni mama wa familia na kutekeleza majukumu yangu ya familia na nitakapokuwa kazini, nitavaa kofia kwa mujibu wa nafasi yangu," alifafanua.

WAFURAHIA UTEUZI WAKE

Baadhi ya mawaziri wanawake wa Zanzibar, walisema mwanamke ni jeshi kubwa katika kuleta maendeleo, hivyo wanampongeza Rais kwa kuwapa kipaumbele wanawake kwa kumteua Zena.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lema Muhamed Mussa, alisema mwanamke ana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya maendeleo kuliko mwanamume.

“Unapomwelimisha mwanamke, umeielimisha jamii nzima, lakini unapomwelimisha mwanamume, unamwelimisha peke yake, hivyo kitendo cha kuteuliwa kwa Zena, kinatupa ari sisi wanawake na kasi ya maendeleo na mabadiliko yatakuwa makubwa," alisifu.

Waziri wa Habari, Vajina na Michezo, Tabia Mwita, alisema uteuzi huo ameupokea kwa furaha na Rais Mwinyi anazidi kujenga imani kwa wananchi kwa sababu anatekeleza yale ambayo aliyaahidi ikiwamo kuwapa nafasi wanawake...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa