Kauli ya CCM Katiba Mpya yashtua upinzani

24Jun 2022
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Kauli ya CCM Katiba Mpya yashtua upinzani

SIKU moja baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusisitiza umuhimu wa kuwapo kwa Katiba Mpya, Chama cha ACT-Wazalendo kimepongeza, huku CHADEMA wakiamua kuitisha kikao cha Kamati Kuu kujadili suala hilo kabla ya kutoa tamko.

Juzi, Katibu wa Halmashauri Kuu wa CCM Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alitangaza CCM kinasisitiza umuhimu huo kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuangalia namna bora ya kufufua na kukwamua mchakato wake.

Akizungumza na Nipashe kuhusu kauli hiyo iliyotokana na vikao vya juu vya chama hicho kikiwamo cha NEC kilichofanyika Dodoma, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema wamewasikia wanzao wa CCM na wamepanga kuitisha kikao cha Kamati Kuu.

“Tumewasikia wenzetu wa CCM kuhusu Katiba Mpya, kwa sasa tutaitisha kikao cha Kamati Kuu na itajadili na hatimaye kutoa tamko lake siku za usoni. Hivyo, tutawajulisha baada ya kikao husika kukaa,” alisema.

Wakati CHADEMA wakijipanga kwa hilo, ACT-Wazalendo walitoa taarifa jana kupitia Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma Taifa, Salim Bimani, kikipongeza kauli hiyo ya CCM.

“Hatua hii ni kubwa, Mwenyekiti wa Taifa wa chama chetu, Juma Duni Haji, amefarijika kuwa mazungumzo yake na viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar yamezingatiwa katika uamuzi huu,” Bimani alisema.

Hata hivyo, Bimani alisema wanatambua kuwa ni lazima kuwapo na mchakato wa kupata mwafaka wa namna ya kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya.

"ACT-Wazalendo tumeshawasilisha mapendekezo yetu kwa Kikosi Kazi cha Rais, tunaamini kikosi kazi kitaratibu maoni na mapendekezo ya vyama vyote na wadau wengine na kuyafikisha serikalini ili mchakato wa Katiba Mpya uanze ifikapo mwezi Oktoba kama tulivyopendekeza," alisema.

Alisema wanatarajia juhudi za kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi zitakwenda sambamba na kuharakisha maridhiano ya Zanzibar.

“Mapendekezo yetu kuhusu maridhiano ya Zanzibar yamewasilishwa kwa mamlaka zote pamoja na Kikosi Kazi cha Rais,” alisema.

Mchakato wa Katiba Mpya ulisimamiwa na iliyokuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu Joseph Warioba, kukiandaliwa rasimu ya Katiba iliyokabidhiwa Desemba 30 mwaka 2013.

Safari ya mchakato wa kupata Katiba Mpya ilianza mwaka 2010 wakati Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, alipoamua kuutangazia umma dhamira na nia ya serikali kuanzisha mchakato huo.

Mchakato ulianza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Habari Kubwa