Kauli ya DC yamnusuru ofisa kutumbuliwa

17Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Muheza
Nipashe
Kauli ya DC yamnusuru ofisa kutumbuliwa

MKUU wa Wilaya ya Muheza, Mwanaasha Tumbo, jana alimnusuru Kaimu Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Salehe Kang’e, kutumbuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula.

MKUU wa Wilaya ya Muheza, Mwanaasha Tumbo, PICHA MTANDAO

Ofisa huyo aliokolwa baada ya mkuu huyo wa wilaya kusema halmashauri haina mtendaji wa sekta ya ardhi anayeweza kuvaa viatu vya ukuu wa idara iwapo anayeshikilia sasa nafasi hiyo ataondolewa.

Hatua hiyo ilitokana na Naibu Waziri kusema ofisa huyo hafai kuendelea kushikilia wadhifa huo kutokana na kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Bakari Mhando, alimwomba Naibu Waziri kutomwondoa katika nafasi hiyo na kubainisha kuwa upungufu aliuonyesha atahakikisha unarekebishwa ndani ya mwezi mmoja.

Akiwa katika ziara ya kushtukiza wilayani Muheza juzi, Mabula alionyesha kuchukizwa na mkuu huyo wa idara kushindwa kusimamia ukusanyaji kodi ya ardhi ikiwamo kutoa hati za madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi katika Wilaya ya Muheza.

Kwa mujibu wa Kang'e, ambaye amebakiza mwaka mmoja kustaafu kazi, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza imeingiza viwanja 3,000 katika mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki na mashamba 1,009, lakini imetoa hati moja ya madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi.

Dk. Mabula alisema alichotegemea baada ya kuingizwa viwanja na mashamba kwenye mfumo huo wa ulipaji kodi kwa njia ya kielektroniki, mkuu wa idara ya ardhi angehakikisha wadaiwa wote sugu wanafuatiliwa ili walipe kodi lakini kinyume chake kazi hiyo haijafanyika na ni mdaiwa mmoja tu aliyepelekewa hati ya madai.

Alisema msisitizo wa serikali ni kuhakikisha inakusanya mapato yakiwamo ya kodi ya ardhi ili kusaidia shughuli za maendeleo ambazo haziwezi kupatikana iwapo serikali haitakuwa na makusanyo mazuri ya kodi.

Kutokana na hali hiyo, Mabula alitoa mwezi mmoja kwa mkuu huyo wa idara kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi wanapelekewa hati za madai na watakaokaidi wafikishwe katika mabaraza ya ardhi na ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kaskazini ifuatilie utekelezaji wa agizo hilo.

Mkuu wa Wilaya, Tumbo, baada ya maelekezo ya Naibu Waziri, alisema atahakikisha utekelezaji  unafanyika na matunda yameanza kuonekana katika baadhi ya maeneo ya  sekta ya ardhi ikiwamo uingizaji wamiliki wa viwanja na mashamba katika mfumo. Alisema suala la hati za madai nalo atalisimamia kikamilifu.

Alisema, changamoto kubwa inayoikabili Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ni kukosekana watendaji wa sekta ya ardhi wenye uwezo mkubwa wa kusimamia masuala ya ardhi na kubainisha kuwa mbali na mkuu wa idara aliyepo sasa, halmashauri hiyo haina watendaji wa kutosha.

Habari Kubwa