Kauli ya IGP kwa Lissu

12Aug 2020
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Kauli ya IGP kwa Lissu

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Simon Sirro, amewaonya wanasiasa walioanza kuonyesha shari kupitia matamshi na sura zao kuelekea uchaguzi mkuu.

Sirro pia amezungumzia maendeleo ya uchunguzi wa jeshi hilo kuhusu shambulio la kupigwa risasi kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

IGP Sirro alizungumzia masuala hayo juzi wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV.

Kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi aliwataka wanasiasa kutolichokoza jeshi hilo na pia wasililaumu litakapochukua hatua dhidi yao.

“Nimeona viongozi wa siasa wanazungumza mambo makali sana. Ninawaheshimu viongozi wote wa siasa katika ngazi zote lakini lazima sheria na kanuni zilizopo ziheshimiwe.

“Ukiangalia baadhi ya viongozi wanavyozungumza unaona kuna ushari. Ushari wanauonyesha wanaupeleka kwa washabiki wao wawe na ushari huo huo. Wao wanachozungumzia si uchaguzi wa amani na utulivu, sera yao ni ushari,” alisema bila kutaja viongozi wala chama cha siasa.

“Niwaombe sana (viongozi wa siasa) anayetaka kufanya siasa afanye siasa, anayetaka kufanya ushari aache mapema. Unamkuta kiongozi mkubwa anazungumza maneno ya ukali sana, anasahau amepata nafasi ya kuzungumza kutokana na amani iliyopo. Kama siyo amani angekuwa chini ya uvungu wa kitanda chake.

“Sheria na taratibu zimewekwa na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), habari ya kusema nimeshazungumza nimemaliza basi hakuna wa kuhoji (anamrejelea kiongozi anayezungumza kwa shari), hii siyo lugha nzuri.

Watanzania wengi wanapenda amani, hawataki shida…lakini wakumbuke kuna maisha baada ya uchaguzi. Uchaguzi utapita na tutaendelea kuishi tuna watoto na wajukuu, tunataka amani na utulivu,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, viongozi wanaoanza na ushari wasilaumu vyombo vya dola kwa kuwa Watanzania wanaona kuna jambo wanalitafuta la ushari.

“Kwa kuwa nina dhamana ya ulinzi na usalama, wanaojiandaa kwa ushari wajue sisi tupo kwa mujibu wa sheria, na wanaozivunja sheria, tukianza kuwashughulikia asitulaumu,” alisema.

Sambamba na hilo, IGP alibainisha kwa Tanzania haiwezi kupata viongozi wazuri katika vurugu bali watapatikana kukiwa na amani tele na kwamba ni vyema viongozi hao wakaendelea kunadi sera zao kuliko kutafuta shari.

Aidha, aliwataka vijana kutojiingiza kwenye mambo yanayofanywa (shari) kwa maslahi ya wachache, na kwamba ni vyema wakaangalia familia zao na maisha kwa ujumla.

Habari Kubwa