Kauli ya Magufuli akichukua fomu kugombea urais

17Jun 2020
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kauli ya Magufuli akichukua fomu kugombea urais

RAIS John Magufuli amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili katika Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma.

RAIS John Magufuli.

Akimkabidhi fomu hizo za urais Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Dk.Bashiru Ally ametoa maelekezo ya namna ya kujazwa kwa fomu hizo.

“Hizi ni fomu kwa ajili ya wadhamini 250 katika mikoa katika mikoa 12 na kati ya mikoa hiyo 12 miwili iwe ya Zanzibar mmoja upande wa Unguja na mwingine upande wa Pemba” amesema Dk.Bashiru

Baada ya kukabidhiwa, Magufuli amezikagua fomu na kuahidi kuafuta wadhamini ndani ya siku 17 ili aweze kurejesha fomu hiyo ili kuendana na matakwa ya kanuni za chama hicho.

''Asante sana Katibu Mkuu, naomba nianze hili zoezi la kutafuta wadhamini kwa Mwenyekiti wa CCM hapa Dodoma naye anidhamini na nitaenda mikoa yote kwa sababu nimekuwa nikipigiwa simu wanataka kunidhamini hivyo naamini nitarejesha fomu yangu kwa wakati'', amesema Magufuli.

Magufuli amesema amechukua fomu hiyo kwaajili ya kuomba nafasi ya kuipeperusha bendara ya CCM pamoja na Ilani nzuri ambayo imeandaliwa kwaajili ya miaka mitano ijayo.

Rais Magufuli amechukua fomu hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya kulivunja bunge la Tanzania na kuwataka wabunge pamoja na watu wengine wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kufanya hivyo huku akionya matusi na vurugu katika kampeni.

Tayari Vyama mbambali vilikwishaanza michakato ya ndani ya kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi za ubunge,udiwani na urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Habari Kubwa