Kauli ya Rais Emerson, Magufuli kifo cha Robert Mugabe

06Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kauli ya Rais Emerson, Magufuli kifo cha Robert Mugabe

Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Rais wa kwanza wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Familia ya rais huyo wa zamani imeiambia BBC kuwa amefariki akipigania afya yake nchini Singapore, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa amemzungumzia Mugabe katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa ni kiongozi shupavu na aliyeongoza vita ya kupinga ukoloni pamoja na kuwapigania watu wake.

“Mchango wake hautasahaulika.” Ni  kauli ya Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa akimzungumzia kifo cha mtangulizi wake, Robert Mugabe. 

Pia katika ukurasa wa Twitter wa Rais wa Tanzania John Magufuli ameandika "Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe, Afrika imepoteza mmoja wa Viongozi Jasiri, Shupavu, Mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa Ukoloni kwa vitendo, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina”- Rais Magufuli

Robert Mugabe alizaliwa Februari 21, 1924 katika nchi iliyojulikana kama Rhodesia ambayo sasa ni taifa la Zimbabwe.

Katika historia yake ya mapambano ya kuipigania nchi hiyo, Mugabe aliwahi kufungwa jela kwa zaidi ya miaka 10 baada ya kuikosoa serikali ya kikoloni ya Rhodesia mwaka 1964.

Mugabe aliong’olewa madarakani katika mapinduzi baridi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo mwaka 2017 na baadaye Mnangagwa aliyekuwa makamu wake wa Rais, aliapishwa kuwa Rais wa Taifa hilo kabla ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2019.

Rais Mugabe alikuwa moja ya viongozi wa Afrika waliokaa madarakani kwa muda mrefu. Ameongoza Taifa hilo kuanzia mwaka 1980 hadi 2017.

Mugabe amezaliwa Februari 21,1924 nchini Zimbambwe  na ameacha mke na watoto watatu.

Habari Kubwa