Kauli ya Sabaya baada ya kuhukumiwa miaka 30 jela

15Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Kauli ya Sabaya baada ya kuhukumiwa miaka 30 jela

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amewataka ndugu zake wasiogope kwani Mungu yupo kazini.

Amezungumza hayo leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 muda mfupi baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

“Ndugu zangu msiogope Mungu yupo kazini” amesema Sabaya.

Agosti 24 mwaka huu, Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura walikamilisha kujitetea mahakamani hapo baada ya Jamhuri kukamilisha mashahidi 11 na vielelezo vinane.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

WASIFU WA OLE SABAYA

Lengai Ole Sabaya amezaliwa 26/12/1986 mkoani Arusha. Amesoma Shahada ya Sayansi katika Elimu Chuo Kikuu cha Mtakatifu John Dodoma (St. John University).

Ole Sabaya aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha na pia aliwahi kushika wadhifa wa Udiwani katika kata ya Sambasha Wilaya ya Arusha Mjini mwaka 2015.

Ole Sabaya aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro tarehe 28 Julai 2018 ya aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, Hayati John Pombe Magufuli.

Sabaya alitenguliwa nafasi hiyo ya ukuu wa Wilaya ya Hai tarehe 13 Mei 2021 na Rais Samia Suluhu Hassan ili kupisha uchunguzi wa makosa yaliyokuwa yakimkabili ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha. Tarehe 15 Oktoba 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha imemhukumu Sabaya na wenzake kifungo cha miaka 30 jela. 

Habari Kubwa