Kaya 5,000 kunufaika msaada wa chakula

23May 2020
Mary Geofrey
Arusha
Nipashe
Kaya 5,000 kunufaika msaada wa chakula

KAYA 5,000 za watu wasiyojiweza, walemavu, yatima na wajane, zinatarajia kunufaika na misaada ya chakula kutoka taasisi ya Nama kupitia washirika wake, Annahl Trust na Nice Tanzania.

Imeelezwa kuwa, misaada hiyo yenye thamani ya Sh. milioni 800, itatolewa kwa wakazi wa Dar es Salaam, Pwani na Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuunga juhudi za serikali katika kukabiliana na janga la corona.

Mratibu wa misaada hiyo wa Taasisi ya Nama, Hamza Jabir, aliwaambia waandishi wa habari jijiji Dar es Salaam jana kuwa misaada hiyo itajumuisha pia msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 500.

"Taasisi hizi zimeamua kushirikiana kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na maambukizo ya Corona kwa Watanzania, hivyo tutatoa msaada wa Sh. bilioni 1.3 unaojumuisha vifaa tiba na chakula kwa familia zisizojiweza," aliahidi.

Jabir alibainisha kuwa, misaada ya chakula watakayotoa ni mchele kilo 10, unga kilo 10, sukari, mafuta, vitakasa mikono na barakoa kwa kila familia yenye uhitaji.

Kuhusu vifaa tiba, alisema watatoa mavazi ya kujikinga kwa watoa huduma (PPE0, Oxymeter, oxygen concentrator, Thermoscanner, vitanda vya chumba cha uangalizi maalum (ICU) na vingine vinavyohitajika kwa kuzingatia miongozo wa serikali na Wizara ya Afya.

"Utekelezaji wa utoaji misaada hii utaanza Mei 27 na kuendelea na kwa mtaa wa Mwananyamala pekee, tutazifikia kaya 200 na tutashirikiana na viongozi wa jamii na serikali hasa katika kuzitambua kaya zinazolengwa katika maeneo yote," alisema.

Mratibu mwenza wa shughuli hiyo, Seleman Abdallah, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwapa ushirikiano.

"Tunaishukuru Taasisi ya Nama Foundation kwa kutambua juhudi za serikali na washirika wake An-Nahl na Nice Tanzania ambao ni wadau wakubwa katika kusaidia jamii.

"Tuendelee kuunga mkono serikali na kupongeza kwa juhudi zake kuisadia jamii na kufikia jamii kubwa ya Watanzania itakapopata uwezo zaidi," Abdallah alisema.

Habari Kubwa