Kaya 7,900 kuhakikiwa

06Aug 2020
Paul Mabeja
Dar es Salaam
Nipashe
Kaya 7,900 kuhakikiwa

KAYA 7,936 wilayani Kondoa zilizokuwamo kwenye kipindi cha kwanza cha mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya tatu chini ya Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF), zinafanyiwa uhakiki ili kubaini kaya hewa na zile zenye wanufaika wasio na sifa.

Uhakiki huo ni sehemu ya utekelezaji agizo la Rais John Magufuli, alilolitoa mapema mwaka huu alipokuwa akizindua kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu.

Rais Magufuli aliagiza kabla ya shughuli zozote za kipindi cha pili kuanza, uhakiki wa walengwa ufanyike nchini kote ili kuondoa kaya zote ambazo zimepoteza sifa.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Kondoa, Donald Jidai, wakati wa mafunzo kwa wawezeshaji kuhusu uhakiki wa walengwa, alisema kaya hizo ni kutoka katika vijiji 63.

Jidai alisema uhakiki huo utatumia teknolojia ya kisasa ambayo itasaidia kupatikana kwa walengwa wenye sifa ambao wanastahili kuendelea na mpango huo katika kipindi cha pili kinachotarajia kuanza hivi karibuni.

“Uhakiki huu tutatumia vishkwambi ambavyo vitatusaidia kupata taarifa sahihi na kubaini walengwa wa kweli. Lakini pia kwa wale ambao watakuwa wamehitimu, wataondolewa kwenye mpango kupisha wengine kwani tayari wameshapata uwezo wa kujikimu na familia zao,” alisema.

Pia alisema pamoja na kutumia mfumo wa kisasa kufanya uhakiki, wawezeshaji wamelishwa viapo ili kutenda haki katika mchakato wote wa uhakiki.

Alisema vigezo vinavyotumika kuwaondoa wanufaika katika mpango huo ni pamoja na mtu kuwa kiongozi wa chama au serikali pia mstaafu katika utumishi.

“Mnufaika aliyekufa ataondolewa kwenye mpango kama alikuwa peke yake bila wategemezi. Lakini kwa yule ambaye alikuwa mkuu wa kaya na amekufa basi atachaguliwa mwingine ili kuwa mwakilishi wa kaya maskini,” alisema.

Aidha Ofisa kutoka TASAF Makao Makuu, Deo Shakiula, alisema ili kutekeleza agizo la Rais Magufuli na pia kuondoa dhana iliyojengeka kwa jamii ya kuwemo walengwa hewa, wataanza utekelezaji kwa kusafisha daftari.

“Mafunzo ambayo yanafanyika yanalenga kujenga uelewa wa pamoja wa namna zoezi hili la uhakiki wa walengwa likavyofanyika” alisema Shakiula.

Habari Kubwa