Kaya itakayozembea kupeleka watoto shule,kliniki kukatwa fedha

05Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Kaya itakayozembea kupeleka watoto shule,kliniki kukatwa fedha

Serikali imesema endapo kaya itashindwa kutimiza masharti ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kuhusu kuhakikisha watoto kuhudhuria shuleni au upelekaji watoto kliniki fedha hizo zitakatwa kama adhabu.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Dk.Mary Mwanjelwa.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Dk.Mary Mwanjelwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kaskazini(CCM) Ramo Makani.

Katika swali lake, Makani amehoji serikali itachukua hatua zipi za makusudi kurekebisha kasoro ambazo zinalalamikiwa na wananchi wa Tunduru ili wananchi wapate kunufaika vema zaidi na huduma za mpango husika.

Akijibu swali hilo,Dk.Mwanjelwa amesema malalamiko ya walengwa kuhusu makato ya fedha kipindi cha malipo, suala hilo wanaendelea kuelimishwa kwanini makato yanatokea.

"Sababu za kukatwa fedha za zao ni kutokana na kutimiza masharti ya kupokea ruzuku hasa kwa kaya zenye watoto walio shuleni na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki ambao ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano,"amesema.

Amebainisha endapo kaya itashindwa kutimiza masharti fedha zitakatwa kama adhabu na kuwaomba wabunge kwenye ziara zao kusaidia kutoa elimu ili kuepusha malalamiko ambayo si ya lazima.

Habari Kubwa