Kazi ya Rais kuutangaza utalii yaanza kuleta fursa

14Sep 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Kazi ya Rais kuutangaza utalii yaanza kuleta fursa

MPANGO wa kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kipindi maalum kinachorekodiwa na Rais Samia Suluhu Hassan maarufu kama ‘Royal Tour’ kwenye vivutio mbalimbali vya utalii nchini, umewavuta mawakala zaidi ya 30 kutoka Marekani, Ufaransa na Lithuania.

Mawakala hao wanatarajia kuja nchini Novemba 23, mwaka huu kwa lengo la kutembea katika maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii kwa ajili ya kuwekeza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya utalii(KITS), Francis Malugu, alisema mawakala hao wamevutiwa kuja nchini baada ya kupata taarifa ya kipindi hicho cha Royal Tour kinachorekodiwa na Rais Samia.

Kwa mujibu wa Malugu, ujio wa mawakala hao umeratibiwa na kampuni hiyo ya Utalii ya KITS na kuishirikisha Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

“Baada ya kuona jitihada za Rais kuitangaza Tanzania kupitia kipindi anachorekodi, tuliwataarifu mawakala wa utalii katika vyama vya utalii duniani ambavyo KITS ni mwanachama wake, na zaidi ya mawakala hao 30 waliomba na kuthibitisha kuja nchini Novemba mwaka huu, huu ni mwanzo mzuri na tunapongeza hatua hii ya Rais kutangaza vivutio na tunaona kazi hii imeanza kuzaa matunda,” alisema Malugu.

Alisema kipindi hicho kilichorekodiwa na Rais Samia, kitasaidia kukuza uwekezaji, kuvutia utalii pamoja na kurahisisha shughuli za utangazaji wa vivutio vya utalii vya Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.

“Na itasaidia pia kuifanya dunia kuitambua Tanzania kama sehemu ya mahsusi ya asili ya dunia ambayo kila mpenda utalii atatamani kuitembelea na tunaamini kupitia njia hiyo, itachangia kwa kiwango kikubwa kukuza uchumi wa nchi kupitia watalii, wawekezaji na wafanyabiashara,” alisema Malugu.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Felix John, alisema kutembelewa na mawakala hao ni fursa kubwa kimkakati katika kufanikisha lengo la kutangaza vivutio vilivyopo nchini kwa kuvutia watalii wasiopungua milioni tano ifikapo mwaka 2025 na kuliingizia taifa dola za Kimarekani zisizopungua bilioni sita.

“Kimkakati hilo ni jambo muhimu kwetu na tunapongeza KITS na wadau wengine wanaoendelea kuhamasisha utalii wetu katika nchi mbalimbali duniani,” alisema John.

Rais Samia alianza kurekodi kipindi hicho maarufu kama ‘Royal Tour’ kwenye maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii na uwekezaji, sanaa na utamaduni vilivyopo nchini Agosti 28, mwaka huu kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa.

Kazi hiyo ya kurekodi kipindi hicho maalum ilianzia visiwani Zanzibar na kufuatiwa na Tanzania Bara.