KCMC yajitosa upandikizaji mbegu uzazi

25Jan 2020
Mary Geofrey
Moshi
Nipashe
KCMC yajitosa upandikizaji mbegu uzazi

KUTOKANA na kukithiri kwa tatizo la wanawake na wanaume kukosa watoto, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (KCMC), inatarajia kuanza huduma ya upandikizaji wa mbegu za uzazi.

Pia, imeeleza kuwa kwa sasa inatoa huduma ya ushauri na tiba kwa wenza wenye tatizo hilo katika kliniki yake maalum ya huduma za uzazi.

Hayo yalielezwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Sarah Urasa, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto katika kampeni ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.

Lengo la kampeni hiyo ni kuangazia mafanikio ya serikali yaliyopatikana katika taasisi hizo kwa miaka minne.

Dk. Urasa alisema kwa sasa wanatoa ushauri na tiba kwa wenza wenye matatizo ya kupata watoto, lakini wanatarajia kuanza kutoa huduma ya upandikizaji mbegu za uzazi za wanaume na uoteshaji wa mayai ya kike.

Alisema lengo ni kusaidia wenza ambao hawana uwezo wa kupata watoto na kwamba wanatarajia kuotesha mayai na mbegu hizo kwa kutumia gesi ya Nitrogen inayozalishwa katika hospitali hiyo.

Alisema kwa sasa wanazalisha mitungi 400 kwa siku ya hewa safi ya Oxygen ya kuwekea wagonjwa wa hospitali hiyo na za jirani na hewa ya Nitrogen kwa ajili ya kuhifadhi sampuli na vioteo vya ngozi na mbegu za uzazi.

"Hewa hii ya Nitrogen tutaitumia kuhifadhi mbegu za kiume tutakazopandikiza kwa wanawake hivi karibuni itakapoanza huduma hii, lakini sehemu nyingine, hewa hii inatumika kwa afya ya wanyama," alisema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika hospitali hiyo, Dk. Benjamin Shayo, alisema nchini takwimu za ongezeko la tatizo hilo zinaonyesha limefika asilimia 10 hadi 15.

Alisema kwa sasa KCMC inatoa huduma ya kliniki mara moja kwa wiki na wanatoa huduma za kuchukua vipimo vya Utrasound, kupima homoni na kutoa huduma za ushauri kwa wenza wanaotafuta watoto.

Alisema huduma hiyo ilianza na watu watano kwa siku hadi kufika watu zaidi ya 10, hali inayoonyesha kuongezeka kwa tatizo.
Dk. Shayo alisema tatizo hilo linawakumba watu wenye umri kuanzia miaka 30 hadi 42, wanaume kwa wanawake.

Alitaja sababu za kuwapo kwa tatizo hilo nchini kuwa ni vichocheo vya homoni kutoka kwenye ubongo hadi kwenye mayai na kizazi kutokuwa na uwezo wa kushika mimba.

Alisema pia kuwa na uvimbe kwenye kizazi kwa wanawake, uke kubana kunakotokana na maumbile na kusababisha mwanamke kushindwa kupokea mbegu za kuzalisha mtoto na kuziba kwa mirija ya uzazi kwa wanawake.

Alisema sababu nyingine ni unywaji wa pombe kwa sababu zinaharibu ubora wa mbegu kwa wanaume na wanawake, hivyo wamekuwa wakishauri watu kuacha unywaji wa pombe kupita kiasi.

Dk. Shayo alisema uwiano wa tatizo hilo kwa wanawake unalingana kwa asilimia 40 kwa kila kundi na asilimia 10 kwa kila kundi hakuna sababu za msingi za tatizo hilo.

"Asilimia 40 kwa wanawake na asilimia 40 kwa wanaume wana tatizo hili, ina maana asilimia 80 tatizo hili linasababishwa na mambo niliyoeleza, lakini asilimia 10 kwa wanawake na 10 kwa wanaume hazina sababu yoyote kwa sababu wanapimwa, hawana tatizo, kwa hiyo tunashindwa kujua ni sababu zipi zinawafanya wakose watoto," alisema.

Alisema pamoja na tiba wanazotoa ikiwamo ya vidonge vya kuzalisha mayai ya kusaidia kupata ujauzito, wanatoa ushauri kwa wenza wenye tatizo la kisaikolojia ikiwamo kuwa na mawazo yaliyopitiliza kunakosababisha kutopata watoto.

Alisema pia wanafanya mazungumzo ya kina kuhusu historia ya familia na historia ya tiba alizoanza kutumia mgonjwa ili kufahamu namna ya kumsaidia.

"Pamoja na tiba, tunakaa na mgonjwa au wenza ili kusikiliza historia yao kabla ya kuanza kuwapa kiini cha tatizo na kusaidia kumpa tiba sahihi na kama ikibainika ana tatizo la kisaikolojia, tunawapa ushauri kuwasaidia kupata mtoto," alisema.

Habari Kubwa