Kenyatta amweleza JPM kukerwa kauli ya Jaguar

03Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kenyatta amweleza JPM kukerwa kauli ya Jaguar

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amemtumia ujumbe maalumu Rais John Magufuli unaoelezea msimamo wa serikali yake, kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dany Kazungu.

Ujumbe huo wa maandishi uliwasilishwa jana na Balozi wa Kenya nchini, Dany Kazungu, na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa niaba ya Rais Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam.

Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu alisema Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake, bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.

Amesema siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana na serikali husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.

“Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kidugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na Wajaluo, hivyo ushirikiano katika masuala ya mbalimbali yakiwamo ya kibiashara na ya kijamii haukwepeki."

Hivyo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani kauli hizo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusababisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika Mashariki hasa ya biashara na ya kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana,” amesisitiza Mheshimiwa Majaliwa.

Waziri Mkuu aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania kamwe haitaruhusu wala kufumbia macho kauli au vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uchochezi dhidi ya nchi jirani ili kulinda na kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake Balozi Kazungu alimshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa bungeni jijini Dodoma, iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge wa Jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo msimamo wa Wakenya na serikali yao.

Balozi Kazungu alisema msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Njagua alitoa matamshi ya kichochezi akiwataka raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya wakiwamo Watanzania waondoke ndani ya saa 24.

Habari Kubwa