Kesi dereva taksi anayedaiwa kumteka MO yapigwa kalenda

12Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi dereva taksi anayedaiwa kumteka MO yapigwa kalenda

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imepiga kalenda kesi inayomkabili dereva taksi mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb (46) ya uhujumu uchumi ikiwamo kusaidia kutendeka uhalifu, kutakatisha Sh. milioni nane na kumteka Mohamed Dewji maarufu kama MO.

Kesi hiyo ilipangwa kutajwa jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Deisy Makakala, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na upande wa Jamhuri unaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa tena Juni 25, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Mapema mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai kuwa kati ya Mei Mosi na Oktoba 10, 2018 mahali tofauti jijini Dar es Salaam na jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwa makusudi alisaidia utendaji makosa ya jinai kwa nia ya kujipatia fedha.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Oktoba 11, 2018 katika hoteli ya Colloseum iliyopo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa pamoja na wenzake ambao hawapo mahakamani walimteka MO kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri.

Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 249 cha kanuni ya adhabu cha 16 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kilichotumika kufungua shtaka ya kumteka MO endapo mshtakiwa atakutwa na hatia atahukumiwa kwenda jela kutumika kifungo cha miaka saba.

Ilidaiwa katika shtaka la tatu kuwa, Julai 10, 2018 eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alitakatisha Sh. 8,000,000 huku akijua zimetokana na genge la uhalifu wa makosa ya kupanga.

Hakimu alisema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa Juni 25, mwaka huu.

Habari Kubwa