Kesi kigogo Rubada yapigwa tena kalenda

21Apr 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kesi kigogo Rubada yapigwa tena kalenda

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imeahirisha kalenda kesi inayomkabili Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (Rubada), Aloyce Masanja, dhidi ya mashtaka ya utakatishaji fedha haramu na wizi wa Sh. milioni 86.

Kesi hiyo iliahirishwa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu Warialwande Lema, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo, baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Joseph Kiula, kuomba mahakama kupanga tarehe ya kutajwa.

Hakimu Lema alisema kesi hiyo itatajwa tena Mei 5, mwaka huu.

Awali, Kiula alidai kuwa kati ya Agosti mosi na 10, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, Masanja akiwa mwajiriwa na mtumishi wa umma, aliiba Sh. milioni 50 zilizomfikia kupitia nafasi yake.

Ilidaiwa katika shtaka la pili, kati ya Novemba 10 na 30, mwaka 2010, mshtakiwa kwa kutumia nafasi yake, aliiba Sh. milioni 36 zilizomfikia kupitia cheo chake.

Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la tatu na la nne kuwa mshtakiwa alitakatisha Sh. milioni 86 baada ya kuziingiza kwenye mchakato wa uhamishaji wa fedha hizo huku akijua ni sehemu ya kosa la wizi.

Mshtakiwa Masanja alikana mashitaka hayo.

Habari Kubwa